WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itatoa msukumo wa kipekee
katika kukamilisha miradi ya kipaumbele na kimkakati inayoendelea kutekelezwa
na Serikali ya Awamu ya Tano ili wananchi waendelee kupata huduma bora.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali
itashirikiana na sekta binafsi kuleta mageuzi kwa kutekeleza kwa kasi mpango wa
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (yaani Blue Print for Business Environment).
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu,
Juni 15, 2020) wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge. Amesema, lengo ni
kuhakikisha shughuli za uchumi na biashara zinashamiri na kuchangia kuondoa
umaskini nchini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga vizuri
kutekeleza mipango yote iliyowekwa katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya
mwaka 2020/2021. “Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii pamoja na
kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama unaimarishwa.”
“Nitoe rai
kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani waendelee kushirikiana na Serikali katika
kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Aidha, natoa wito kwa sekta
binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote waendelee kutoa ushirikiano katika
utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.”
Waziri Mkuu amesema, Serikali
itaendelea kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 kwa
kuzingatia athari na changamoto za ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa
na virusi vya Corona (COVID-19).
Pia, Waziri Mkuu
amesema Serikali itakamilisha mchakato wa shughuli zilizobaki za maandalizi ya
uchaguzi mkuu wa ubunge, urais na udiwani na kuiwezesha Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kusimamia kikamilifu shughuli zote za uchaguzi huo kwa uhuru na haki.
Amesema sambamba
na maandalizi ya uchaguzi mkuu, utekelezaji wa kazi za Serikali utaendelea. “Hivyo,
watumishi wote wa umma wanashauriwa waendelee kutekeleza majukumu yao kwa
weledi, uaminifu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi na tija wakati
wote.”
Wabunge
wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 ya jumla ya sh.
trilioni 34.88, kati ya fedha hizo, sh. trilioni 21.98 ni za matumizi ya
kawaida na sh. trilioni 12.90 ni za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 37 ya
bajeti yote.
No comments:
Post a Comment