Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kushoto) na Mkuu
wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga kuelekea kuzungumza na watendaji wa sekta
ya ardhi katika mkoa wa Geita wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta
ya ardhi mwishoni mwa wiki.
Na Munir Shemwta, WANMM GEITA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini
kupitia idara zake za ardhi kuhakikisha zinapima maeneo yote yenye migodi ili kuondokana
na migogoro.
Dkt Mabula alisema hayo
mwishoni mwa wiki aipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa
Geita akiwa katika ziara ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi pamoja na
utekelezaji wa miradi inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa
humo.
Dkt Mabula alisema, mkoa
wa Geita una migodi mingi bila kuwa na suala la upimaji na umilikishaji maeneo
ya Migodi migogoro kwenye maeneo hayo haitaisha kwa kuwa leseni ya uendeshaji
shughuli za uchimbaji madini inaonesha umiliki eneo la chini lenye madini.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitolea mfano wa Mgodi wa Madini wa Nyamongo kuwa,
umefanikiwa kupima maeneo yake na sasa mgodi huo pamoja na kuwa na haki ya
umiliki eneo la chini la madini (mineral rights) lakini Mgodi huo inamiliki pia
eneo la juu (surface rights) na hivyo kuondokana na migogoro.
‘’Hakikisheni wanaoendesha
shughuli za migodi wanamiliki kihalali maeneo yao, ana surface rights na ana
minerals rights ili awe salama habari ya kufukuzana na watu wanaopita juu
haipendezi, ana haki ya kuwa pale juu kwa sababu wewe leseni yako ni ya kule
chini sasa wewe unaniondoaje’’ alisema dkt mabula
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, kwa bahati nzuri kwa sasa wachimbaji wadogo nao tayari wameanza kuanishiwa
maeneo hivyo kasi ya kuyapima maeneo hayo iongezeke ili wanaoendesha shughuli
za migodi wamiliki kihalali maeneo yao sambamba na kuongeza wigo wa makusanyo ya
kodi ya ardhi kwa serikali.
Amewataka watendaji wa
sekta ya ardhi katika maeneo yenye migodi kuangalia namna bora ya kuzungumza na
wamiliki hao ili kutambua umuhimu na faida ya kupima maeneo yao kwa lengo la kuondokana
na mgogoro.
Akiwa katika wilaya ya
Chato ambako alikagua pia mradi wa ujenzi wa ofisi ya Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) Biharamulo unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),
Dkt Mabula ameitaka wilaya hiyo kuandaa mpango wa mji huo ili kuwa na sura ya
kitalii na kusisitiza utolewaji elimu kwa viongozi wa vijiji kuwaelekeza
wananchi umuhimu wa kujenga nyumba kwa mpangilio ili kuepuka ujenzi holela
Naibu Waziri Mabula
aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Chato kufuatilia
wananchi wasijenge kiholela na kubainisha kuwa NHC inaweza kutumika katika kupanga
miji kupitia ujenzi wa nyumba zake ili kuzuia ujenzi holela.
No comments:
Post a Comment