HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 12, 2020

Rais Magufuli amsamehe Andengenye

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akitazama kibao cha Ufunguzi mara baada ya kufungua Jengo la Ofisi za Makao
Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

 

Dodoma, Tanzania

Rais John Magufuli ametangaza kumsamehe aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye na kusema kuwa hatamrudisha ndani ya jeshi hilo bali atamtafutia kazi nyingine.

Rais Magufuli ametangaza msamaha huo jana mkoani Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini
mkoani humo. 

Alisema amefikia hatua hiyo baada ya Andengeye kumwomba radhi mara nyingi, hivyo ameamua kumsamehe lakini hatamrudisha katika jeshi hilo badala yake atamtafutia kazi nyingine.

“Sisi wote ni wadhambi unapomwona mtu anaonesha dalili za kutubu, msamaha lazima uwepo, hata aliyekuwa Kamishna wenu wa Jeshi la Zimamoto (Andengenye) nimemsamehe ila simrudishi ‘fire’ lakini namtafutia kazi nyingine, ameniomba msamaha mara nyingi.

“Mliopo hapa mkafikishie salamu kwamba nimemsamehe na hapa kwa sababu ameomba msamaha zaidi ya mara tatu, ni unyenyekevu wa aina yake, lakini kwenye jeshi hili hatarudi mtamuona katika maeneo mengine,” alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufulii alisema viongozi waliopo sasa katika jeshi hilo wameufanyia marekebisho mkataba uliomfanya Andengenye kuondoka kwenye nafasi yake hivyo anawataka maofisi wa jeshi hilo kuwa waaminifu na fedha za umma kwa kuwa katika uongozi wake hakuna fedha za bure. “Fedha za bure katika kipindi changu ni mbaya zitawaharibia maisha yenu
na mimi hata mloge namna gani sibadiliki, niwaombe ndugu zangu wa Zimamoto yaliyopita si ndwele tuyasahau na tusiyarudie,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli ametoa msamaha kwa makamishna wengine wa jeshi hilo ambao alipelekewa mapendekezo ya kuwashusha vyeo na kuwaondoa ndani ya jeshi hilo.

Alisema anafahamu kuwa kulikuwa na mapendekezo ya makamishna kama wanne kuwateremsha cheo na wengine kuwafukuza, ameangalia wanavyopendeza, walivyo na huruma na nyuso zao zinaonesha wametubu, Msamaha wa Rais Magufuli umekuja kufatia na Andengenye kuondolewa
katika wadhifa wa Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo kutokana sakata la mkataba tata wa ununuzi wa vifaa vya uoakoaji, wenye thamani ya zaidi ya Sh. Trilioni moja.

Kamishna Andengenye alifutwa kazi na Rais Magufuli Januai 23 mwaka huu katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za askari Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.

Mbali na Andengenye, mwingine aliyeng’oka kutokana na sakata hilo ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Kangi Lugola.

Rais Magufuli aliwatuhumu viongozi hao kutosimamia masilahi ya nchi wakati wanafanya makubaliano ya mkataba huo baina ya Tanzania na kampuni ya kigeni iliyopewa zabuni ya uuzaji wa vifaa hivyo.
 
Licha ya kuwaondoa kwenye nyadhifa zao, Rais Magufuli aliagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi dhidi ya sakata hilo, ambapo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), ilitekeleza agizo hilo. 

Februari 21, mwaka huu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo, alisema baada ya kukamilisha uchunguzi wao wamebaini mashtaka yanayowakabili ni ya uhujumu uchumi hivyo watapeleka jalada hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.

No comments:

Post a Comment

Pages