Ofisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Patrick Massawe, akimuelimisha mfanyabiashara wa eneo la Karuta mkoani Mwanza kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea jijini humo. (Picha na Veronica Kazimoto).
Na Veronica Kazimoto, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya kampeni ya elimu kwa
mlipakodi inayoendelea mkoani hapa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku wafanyabiashara hao wakiishukuru
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa zoezi hilo ambalo linawaleta karibu
walipakodi na wakusanya kodi.
Akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu kampeni hiyo ambayo imeanza June 15 hadi 22 mwaka huu, Mkuu wa
Mkoa huyo amesema kuwa, ni muhimu wafanyabiashara wote wakalipa kipaumbele
suala la ulipaji kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za
jamii kwa manufaa ya kila Mtanzania.
“Kama mnavyojua umuhimu
wa kodi na hasa katika kipindi hiki cha awamu ya tano hakuna Mtanzania ambaye hajashuhudia umuhimu wa kodi, tumeona barabara zikijengwa, ndege zikinunuliwa, ujenzi
wa vituo vya afya, meli zikijengwa, ukarabati wa viwanja vya ndege ambavyo
vyote vimesababishwa na uwezo wa serikali ambao umejengeka kwa mapato ya ndani,”
alisema Mongella.
Mongella amesema kwamba,
kutokana na faida hizo za kodi, ni muhimu wafanyabiashara wote wakatoa
ushirikiano kwa maafisa hao wa TRA watakaopita katika maeneo ya biashara zao wakifanya
zoezi hili la kutoa elimu ya kodi na kutumia fursa hiyo kupata uelewa na hatimaye
waweze kulipa kodi ipasavyo na kwa wakati.
Amesema zoezi hilo
limelenga kuwafikia wananchi na wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali mkoani
hapa yakiwemo Rwagasore, Pamba road, Buhongwa, Nyerere road, Misungwi, Mwaloni
na Kisesa.
Sambamba na hayo amesema
mambo yote yamefanikiwa kutokana na uadilifu na utendaji kazi wenye tija
uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kusimamia mapato ya ndani na
kuyaelekeza katika kuimarisha uchumi wa nchi.
Frola Ayo ambaye ni
mfanyabiashara wa mapambo na Charles Lyamuya mfanyabiashara wa duka la vifaa
vya ujenzi ni baadhi ya walipakodi waliopo Mtaa wa Lumumba na Karuta jijini
hapa ambapo wameomba zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi liwe endelevu kwani linajenga
urafiki baina yao na TRA na hivyo litaongeza uhiari wa kulipa kodi kwa wakati.
"Kutokana na elimu
hii hakika tutalipa kodi ipasavyo kwa sababu inatuweka karibu na TRA suala
ambalo linatuondolea hofu na pia tunaomba elimu hii iwe endelevu ili wafanyabiashara
wengi waweze kujijenga zaidi na kuimarika katika biashara zao,” alisema
Lyamuya.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi
inayoendelea mkoani Mwanza inafanyika pia katika Mkoa wa Morogoro na Mbeya na imelenga
kuwaelimisha walipakodi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja
na kupokea maoni, kusikiliza kero na changamoto za walipakodi hao ili kuzitafutia
ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment