HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 14, 2020

Taasisi za umma zatakiwa kudumisha ushirikiano

Dk. Mary Mwanjelwa.   

NA JAMES MWANAMYOTO, DODOMA

 
TAASISI za umma nchini zimeelekezwa kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 kwa kudumisha ushirikiano na wananchi na wadau, ili kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia Mikataba ya Huduma kwa Mteja.

Maelekezo hayo yametolewa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora . Dk. Mary Mwanjelwa (pichani).

Dk. Mwanjelwa alisema, ushirikiano na wadau ni sehemu ya utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu ambayo inasisitiza jukumu la Utumishi wa Umma katika kujenga na kudumisha amani iliyopo miongoni mwa jamii.

"Katika mwendelezo wa kutekeleza Kauli Mbiu, naziagiza taasisi zote za umma kuadhimisha wiki hii kwa kufanya shughuli za kijamii katika maeneo ambayo wananchi wanapata huduma husani kwenye hospitali, masoko na maeneo mengineyo kwa kuzingatia tahadhari dhidi ya corona, kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri yatakayowezesha utendaji kazi wa taasisi za umma, " alisisitiza.

Aliongeza kuwa, Watendaji wa Taasisi za Umma wanatakiwa kuadhimisha wiki hii kwa kukutana na watumishi katika maeneo yao ya kazi ili kusikiliza maoni na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mwanjelwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kutumia maadhimisho haya kujitathmini kama wanaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kwa dhati kuboresha huduma zitolewazo na Taasisi za Umma kwa wananchi  na hatimaye kuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, Dk. Mwanjelwa ameziagiza Taasisi za Umma kuwasilisha taarifa ya namna walivyoshiriki maadhimisho hayo Ofisi ya Rais Utumishi mara baada ya kilele cha maadhimisho ili kuiwezesha Serikali kutumia taarifa hizo kufanya tathmini na kuboresha utendaji kazi.

Sanjali na hilo, aliwapongeza Watumishi wote wa Umma kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo pamoja na changamoto za maambukizi ya Homa kali ya mapafu kuwepo.

Naibu Waziri aliwahakikishia Watumishi wa Umma kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inawathamini na iko pamoja nao, hivyo amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa manufaa na maendeleo ya taifa kama Rais Dk. John Magufuli anavyosisitiza kupitia kaulimbiu yake ya “HAPA KAZI TU” ambayo imekuwa ni chachu katika kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi kwenye Taasisi za Umma.

Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuanzia Juni 16 hadi 23 kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU) ni “Jukumu la Utumishi wa Umma katika Kujenga na Kudumisha Amani iliyopo Miongoni mwa Jamii.

No comments:

Post a Comment

Pages