Mdau wa maendeleo, Brighton Armi, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali kama mashine za kunawihia mikono,
vitakasa mikono na ndoo maalum za kunawa kwa uongozi wa kijiji cha
Malolo kilichoko wilaya ya Kilosa.
Mdau
wa maendeleo, Brighton Armi, akimkabidhi afisa mtendaji wa kijiji,
Ferdinand Weteka baadhi ya vitu alivyokabidhi kwa ajili ya kituo kipya
cha afya cha kijiji cha Malolo na shule za msingi na sekondari za kijiji
hicho.
Na Denis Mlowe, Kilosa
JAMII ya wafugaji na wakulima nchini wametakiwa
kudumisha upendo na ushirikiano kuepusha migogoro ya mara kwa mara kwa lengo la
kudumisha amani katika maeneo wanayoishi.
Ushauri huo umetolewa na mwanajamii mfugaji ,Brighton Armi mdau wa maendeleo
ambaye anasoma nchini Ujerumani wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa
ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona kwa kijiji cha Malolo
kilichoko wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Akizungumza kabla
ya kukabidhi msaada huo uliotolewa na taasisi ya Ghoada Asseta anayomiliki,
Armi alisema kuwa jamii za wafugaji na wakulima wamekuwa wakipata changamoto
kutokana na mwingiliano wa ardhi hivyo upendo na ushirikiano ndio njia pekee ya
kuepuka migogoro hiyo nchini.
Alisema kuwa msaada huo una lengo la kuwakutanisha
pamoja jamii hizo hasa katika kipindi hiki cha pambano dhidi ya kuenea kwa
virusi vya corona ambalo ni janga la dunia hali iliyomlazimu kutumia misaada
hiyo kudumisha upendo na ushirikiano miongoni mwao.
Alisema kuwa corona ipo na imegusa dunia nzima na hivyo
masuala ya maendeleo lazima yaendelee kwa watu kufanya kazi kama ambavyo Rais
Magufuli anasisitiza watu kufanya kazi hivyo lazima kujenga uhusiano mzuri
katika jamii inayotuzunguka.
Armi alisema kuwa hali ya migogoro miongoni wa jamii
za ufugaji na wakulima ikiendelea maendeleo hayatakuwepo zaidi kutakuwa na
mapambano ambayo hayana faida kwa jamii na kudumaza maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa katika kuwafanya jamii ya Malolo
kufanya kazi kwa ushirikiano huku wakipambana na kuenea kwa virusi vya corona ameamua kutoa msaada wa vitakasa mikono ,
mashine za kisasa za kutoa maji yanayotiririka kwa ajili ya shule za kijiji
hicho, ndoo, vazi maalum kwa ajili ya wauguzi, mashine ya kupimia joto la
binadamu na na barakoa vyote vikiwa na thamani y ash. Milioni 6.5
Akipokea vifaa hivyo afisa mtendaji wa kata ya Malolo, Ferdinand Weteka
kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kilosa, alisema kuwa kwa msaada huo ambao
umetolewa na Brighton Armi vifaa kinga hivyo vitawajengea ujasiri watoa
huduma za afya katika kijiji hicho na kuwasaidia wanafunzi kuweza kujinga zaidi
dhidi ya pambano ya kuenea kwa virusi vya Corona.
Alisema kuwa katika kijiji hicho hakuna kesi yoyote wala
tetesi za kuwepo kwa mgonjwa wa virusi vya corona hivyo msaada huo umekuja
katika wakati mwafaka na kumshukuru kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho na
kutoa wito kwa wadau wengine kuangaza macho yao kwa wananchi wanaoishi
vijijini.
Naye Afisa Elimu kata ya Malolo, Rehema Mwinuka alisema
wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali za kuhakikisha wanafunzi waliofungua
shule wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa
wa COVID 19 kwa kutoa elimu ya namna ya
kujikinga, huku akiongeza kuwa kijiji cha Malolo kipo vizuri na wananchi wengi
wanaelimu ya pambano dhidi ya kuenea kwake.
Amemshukuru Armi kwa kuwa msaada mkubwa kwenye shughuli za
maendeleo katika kijiji hicho na kuwa mfano bora kwa jamii aliyokulia na
kuzaliwa kwani ameonyesha njia na faida ya elimu kwa vijana wengi kutoka
kijijini hapo.
No comments:
Post a Comment