Balozi Seif Ali Iddi akizishauri
Kampuni na Taasisi za Kizalendo zinazopewa Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi ni
vyema zikazingatia kuheshimu Mikataba inayojenga uaminifu.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda
Balozi Seif Ali Iddi akimtwisha Ndoo ya Maji Mkaazi wa Kijiji cha Mahonda Bibi
Pili Mkuya Salum baada ya kuzindua Rasmi Kisima cha Maji safi na salama katika
eneo hilo kilichojengwa na ufadhili wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yardin.
Na Mwandishi Maalumu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amesema Wahandisi wa Ujenzi Wazalendo lazima wajenge Heshima wakati wa
kutekeleza Miradi wanayokabidhiwa katika misingi ya uaminifu kitendo kitachowajengea
SIFA na hatimae kuaminika zaidi.
Alisema wapo baadhi ya Wataalamu Wazalendo wenye tabia chafu isiyokubalika ya kuwadanganya
Viongozi pamoja na Taasisi zilizowakabidhi Miradi ya Ujenzi bila ya kujali
kwamba wametia saini Mkataba unaowapa wajibu wa kuutekeleza kwa muda muwafaka.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya
ziara fupi ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la kuhifadhia
Maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope Mbaleni ambao ulichelewa
kukamilika katika muda uliopangwa ambapo alilazimika kumuagiza Mkuu wa Wilaya
ya Kaskazini “B” kuchukuwa hatua zinazostahiki dhidi ya Wahandisi wa Ujenzi wa
Mradi huo.
Alisema Wahandisi Wazalendo ni vyema wakazingatia
umuhimu na fursa wanazopewa na Serikali pamoja na Taasisi za Kijamii za
kusimamia Miradi ya Maendeleo na
Kiuchumi kwa vile Taifa limeshaanza kuridhika na Taalum zao badala ya ile tabia
ya kuwakumbatia Wahandisi wa Kigeni
“ Baadhi ya Wakandarasi wetu wanatuangusha jambo
ambalo haipendezi hata kidogo kwa vite Taifa tayari limeshajipanga kuwatumia Wataalamu Wazawa katiak shughuli za
Uhandisi badala ya wale waliozoeleka wa Kigeni wanaotumia gharama kubwa”.
Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na
kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” kwa usimamizi mzuri wa Mradi huo
uliokuwa ukisuasua katika utekelezaji wake.
Balozi Seif
alisema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo uliopata nguvu za ufadhili ni
kuwaondoshea usumbufu wa upatikanaji wa huduma za Maji safi na Salama Wananchi
wanaozunguumka eneo hilo ambao wamekuwa wakitumia maji yasiyo salama kwa muda
mrefu.
Akitoa Taarifa ya Mradi huo Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Youth
Icon inayosimamia Ujenzi huo kwa ufadhili wa Taasisi moja ya Umoja wa Mataifa
Bwana Abdullah Suleiman alisema jumla ya Shilingi Milioni 10,000,000 tayari
zimeshalipwa katika Awamu ya pili ya Mradi huo.
Nd. Abdullah Suleiman alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba salio lililobaki litamalizwa mara tu pale Mradi huo
muhimu kwa Maisha ya Wananchi utakapokamilika na kukabidhiwa Rasmi kwa Wahusika
ambao ni Serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Rajab Ali
Rajab alisema alilazimika kumpa agizo la kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Kaskazini “B” Asubuhi ya Ijumaa ya Tarehe17 Aprili Mwaka huu Mkurugenzi wa
Kampuni ya Grative Tanzania Limited yenye Makao Makuu yake Dar es salaam kutoa
maelezo ya kina kuhusiana na kuchelewa kumalizika kwa wakati Mradi huo.
Nd. Rajab alimueleza Balozi Seif kwamba Agizo hilo
lilitanguliwa na lile alilompa Mhandisi wa usimamizi wa Ujenzi huo aliyepo
Zanzibar la kumtaka asitoke nje ya Zanzibar na kuripoti kwa Mkuu wa Polisi
Wilaya kila Jumatatu saa 3.00 asubuhi agizo analoendelea kulitekeleza hadi
Mradi huo utakapokamilika Rasmi.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” alisema
makubaliano ya kukamilika kwa Mradi huo kati ya Uongozi wa Serikali ya Wilaya
hiyo na Uongozi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yamefikiwa ambapo
ifikapo Tarehe 25 Juni Mradi huo utakabidhiwa rasmi.
Nd. Rajab alifahamisha kwamba kukamilika kwa Mradi
huo ambao kwa sasa uko katika hatua ya kumaliza Zege kwenye Tangi la juu la
kuhifadhia Maji kutafuatia hatua ya Mamlaka ya Maji Zanzibar kumalizia
miundombinu ya uingizaji wa huduma hiyo ili baadae iwafikie Wananchi
waliokusudiwa.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alizindua Rasmi Kisima cha Maji Safi na salama
kilichojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mahonda kwa Ufadhili wa Taasisi ya Misaada
ya Hayrat Yardin kilichopo Magharibi ya Skuli ya Mahonda.
Kisima hicho kilichoanza kujengwa mnamo Tarehe 9
Disemba 2019 hadi Tarehe 7 Januari 2020 kwa kuhudumia Zaidi ya Wananchi Mia
Tatu wanaokizunguuka kimegharimu jumla ya Dola za Kimarekani Elfu Nne sawa na
Shilingi za Kitanzania Zaidi ya Milioni Tisa.
Akizungumza na Wananchi wa eneo hilo Balozi Seif
ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwashukuru na kuwapongeza
Viongozi na Watendaji wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yarnid kwa kuguswa na changamoto iliyokuwa
ikiwakabili Wananchi wa Mahonda ya ukosefu wa hudum hiyo muhimu.
“ Eneo la Mahonda limekuwa na changamoto kubwa ya
upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama kwa muda mrefu hali inayowapa
Viongozi wa Jimbo fikra za kubuni mipango ya kuwaondoshea changamoto hiyo
Wananchi wake”.Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif alifahamisha
kwamba Maji ni huduma muhimu anayolazimika Kiumbe kuipata katika mazingira yake
ya kawaida yoyote hasa Mwanaadamu ili kustawisha Uhai na Afya yake.
No comments:
Post a Comment