Watanzania sasa wanaweza kufanya malipo ya kodi na yasiyo ya kodi kwenda
kwa taasisi zaidi ya 600 za serikali wakiwa ndani ya matawi yote ya Benki ya
UBA kwa haraka zaidi, imeelezwa.
Hili imetokana na uamuzi wa Serikali kuiunganisha Benki ya UBA na mfumo wa malipo wa Serikali wa kielektroniki (GePG).
UBA ilitangaza jijini Dar es Salaam jana kuwa imepata kibali cha kuwa
moja kati ya benki nane nchini zinazotumika katika kufanya malipo ya kodi na
yasiyo ya kodi kwenda kwa taasisi za serikali kupitia mfumo wa GePG.
Mkuu wa Kitengo cha Sekta ya Umma wa Benki ya UBA, Dominick Timothy, alisema kuwa kuunganishwa
kwa benki yake katika mfumo wa GePG ni moja wapo ya njia za taasisi hiyo ya
fedha kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania,
chini ya Rais John Magufuli.
Alisema kutokana na
kuunganishwa kwa UBA na mfumo wa GePG, Benki hiyo sasa itaoanisha mfumo huo na njia
zake za kidijitali zakibenki.
Njia hizo ni pamoja
na kupata huduma za benki kwa njia ya simu (Mobile App), huduma za benki kwa
njia ya mtandao (internet banking) pamoja na njia zijulikanazo kama Leo chatbot,
USSD Magic Banking na Webcollect.
Lengo la
kuunganisha na njia hizo zakibenki ni ili kuwawezesha Watanzania kuweza kufanya
malipo ya serikali popote pale walipo pasipo kulazimishwa kwenda katika tawi la
benki.
“Siku zote, hamu
yetu imekuwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo
Watanzania. Kwa njia hii, tunaunga mkono juhudi za serikali katika kukusanya
mapato kwa njia za kidijitali. Tunaishukuru Serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato
Tanzania na Wizara nzima ya Fedha na Mipango kwa kutupatia nafasi hii ya
kuwatumikia Watanzania,” alisema.
Alisema mtu yeyote
anaweza kufanya malipo ya serikali kwa njia ya GePG bila kujali kama ni mteja
wa Benki ya UBA au laa.
Mfumo wa GePG unasaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha
za Umma.
Faida za mfumo huo kwa taasisi za umma ni pamoja na
urahisi katika usuluhishi wa
miamala na usuluhishi wa
taarifa za kibenki pamoja na kupata taarifa sahihi na kwa wakati
zinazohusu makusanyo.
Mfumo pia unapunguza gharama za miamala inayohusu
ukusanyaji wa Fedha za Umma.
Serikali ilianza
kutumia mfumo wa GePG mwaka 2017 ikiwa ni njia moja wapo ya Serikali, chini ya
Rais Magufuli, kudhibiti upotevu wa pesa za umma.
Benki ya UBA
imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuiendeleza
Tanzania ambapo mwaka jana benki hiyo ilijiunga na benki nyingine kutoa dhamana
za benki ili
kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji.
Mradi
huo wenye thamani ya $2.95 billion utafua umeme wa Megawati 2,115.
No comments:
Post a Comment