HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 29, 2020

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWAPIGA MSASA WATAALAMU WA UGAVI NA MANUNUZI

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Honest Ngowi, akifungua mafunzo ya wataalamu wa Ugavi na Manunuzi juu ya mabadiliko ya kiteknolojia katika sekta hiyo.


Mshiriki wa mafunzo ya wataalamu wa Ugavi na Manunuzi, Emmanuel Tungo, akichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Honest Ngowi, akitoa mada wakati wa mafunzo ya wataalamu wa Ugavi na Manunuzi.
Mwakilishi Mkazi wa Kuehne Foundation, Beatrice Millu, akizungumza na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Honest Ngowi.
Mshauri wa Ugavi wa Kampuni ya MGT Consultant, Bosco Mapunda, akichangia mada.
Meneja wa Shirika la Posta Kanda ya Dar es Salaam, Simon Bikaru, akichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki.



DAR ES SALAAM, TANZANIA

CHUO Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam kimetoa mafunzo kuwanoa wataalamu wa Ugavi na Manunuzi, juu ya mabadiliko ya kiteknolojia katika sekta ya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mhadhiri Mwandamizi chuo hicho, ambaye pia ni Mratibu wa  Mradi wa Kuehne Foundation, Dk. Omari Swalehe, amesema kuwa mabadiliko ya Teknolojia ni makubwa, hivyo wataalamu wa Ugavi na Manunuzi nao lazima waendane mabadiliko hayo.

Dk. Omari amesema kuwa wateja wanabadilika, huku sheria, mifumo pamoja na kanuni nazo zinabadilika, hivyo ni muhimu kwa Wataalamu wa Ugavi na Manunuzi nao kubadilika pia.

"Wateja ndio wanaamua wanataka nini, wanahitaji bidhaa gani, kwahiyo kampuni nazo lazima zijue mahitaji ya wateja wao kuendana na Teknolojia inavyoelekea," amesema Dk. Omari.

Hata hivyo amesema kuwa taasisi na wataalamu lazima wabadilishe mtazamo wao katika masuala mazima ya Ugavi na Manunuzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Profesa Honest Ngowi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Wataalamu hao, amesema kuwa mambo mengi yanakwenda kidijitali, hivyo walaji wengi wamehamia mtandaoni.

"Walaji na wateja wengi wananunua bidhaa mtandaoni, iwe muziki, nguo na vitu mbalimbali, kwa hiyo Kampuni za Ugavi na Manunuzi pamoja na wataalamu ni muhimu kubadilika kuendana na mahitaji ya wateja," amesema Profesa Ngowi.

Licha ya hilo, Profesa Ngowi amesema kuwa changamoto kubwa kampuni zishindwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, hivyo amewaasa kuendana na mabadiliko hayo ili kufanya biashara na wateja wanaobadilika na mfumo wa manunuzi.

Mwakilishi Mkazi wa Kuehne Foundation, Beatrice Millu, amesema kuwa wito umetolewa kwa wataalamu wa ugavi na manunuzi pamoja na kampuni mbalimbali kuendana na mabadiliko ya uongozi na teknolojia inakoelekea.

Wataalamu waliopata mafunzo ya mabadiliko ya mfumo wa uongozi katika Ugavi  na Manunuzi ni kutoka Taasisi za Serikali, Binafsi, Taasisi za elimu pamoja na wanafunzi wanaosoma masuala ya Ugavi na Manunuzi.

Amesema kuwa wameshafanya semina mbalimbali kwa ajili ya kuwajengea uwezo wadau wa ugavi, kwani kumekuwa na mafanikio makubwa na kuwa washiriki wanajitokeza kwa wingi.

"Katika kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe, tumeona ushiriki umekuwa mzuri, kwani tumepata washiriki wengi na mafunzo yanaonesha mlengo chanya katika masuala mazima ya Mabadiliko katika Manunuzi na Ugavi," amesema Beatrice.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

Pages