HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 05, 2020

GBT YAIKABIDHI TANTRADE VIFAA VYA KUJIKINGA NA VIRUSI VYA CORONA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya michezo ya Kubahatisha, James Mbalwe (kushoto), akikabidhi kwa Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Mohamed, vifaa vya kujikinga na virusi vya corona.



Na Tatu Mohamed

KATIKA kuendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, Bodi ya michezo ya kubahatisha (GBT), imekabidhi msaada wa matanki 10 pamoja na sanitaiza kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika leo Julai 5, 2020 katika viwanja vya maonesho ya 44 ya Biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam 'Sabasaba', Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, James Mbalwe amesema kuwa pamoja na majukumu mengine, pia wanajukumu la kuhakikisha wanailinda jamii.

"Kwahiyo tukaona tushirikiane na Tantrade, kwa kuilinda jamii isiambukizwe na Corona kwasababu tunajua ugonjwa huu bado upo na unaua. Sisi tumeguswa sana tukaona tutumie fursa hii ya kusaidiana na wenzetu ili tuhusike kwa namna moja au nyingine kudhibiti ugonjwa huu.

"Ndio maana tumeleta vifaa vichache, havitaweza kukidhi mahitaji ya jamii inayokuja hapa lakini nafikiri tutaacha alama fulani ili watu wetu wasipate maambukizi. Kwahiyo nichukue fursa hii kuwaambia watanzania watembelee maonesho haya wasiwe na wasiwasi," amesema.

Aidha amesema pia  wameanzisha, kampeni ya kumlinda mtoto kuhakikisha hashiriki michezo hiyo ya kubahatisha mpaka akiwa na umri chini ya miaka 18.

"Nichukue nafasi hii niwaombe watanzania waikumbatie kampeni yetu kwa kutokuwaruhusu watoto wadogo wasishiriki michezo hii.

"Tunajua ni burudani watoto wangependa kushiriki lakini wasubiri muda wao, utakavyofika wataweza kushiriki na kuburudika kama ilivyo kwa watu wazima," amesema.

Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Tantrade, Latifa Khamis ameshukuru kwa msaada huo na kusema kuwa umekuja kwa wakati muafaka.

"Tunashukuru sana kwa msaada huu kwani umekuja wakati muafaka ambapo kuna tukio la kitaifa la maonesho ya sabasaba ambayo yamejumuisha wadau wote. Wametupatia vifaa ambavyo sisi tutaweza vitaweza kutusaidia katika kujikinga na maambukizi haya...kwahiyo tunawashukuru sana," amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages