HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2020

HOSPITALI YA BUGANDO KWA KUSHIRIKIANA NA MOI KUFANYA UPIMAJI WA BURE

 Baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando wakizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (DITF).



Na Janet Jovin

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Bugando Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), wanatarajia kufanya upimaji na uchunguzi bure kwa watu wenye magonjwa mbalimbali yanayohusu nyonga na magoti.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika viwanja vya maonesho ya 44 biashara ya kimataifa, Ofisa Habari wa Hospitali ya Bugando, Lucy Mogele anasema huduma hiyo itatolewa Julai 6, mwaka huu katika hospitali hiyo iliyopo jijini Mwanza kuanzia saa 2 asubuhi hadi 11 jioni.

Anasema kuanzia Julai 7 hadi 11 mwaka huu hospitali hiyo itafanya matibabu ya upasuaji yanayohusiana na kubadilisha nyonga na magoti yaliyoathirika na kuongeza kuwa wananchi watakaotaka kupata  huduma hiyo watatakiwa kuchangia kiasi cha fedha.

"Huduma hizo zote zitafanywa katika hospitali ya Bugando na madaktari Bingwa wa mifupa kutoka MOI, vipimo vitafanyika bure na wale watakaobainika kuwa na matatizo watafanyiwa upasuaji ambao wanapaswa kuchangia kiasi cha fedha," anasema.

Anasema pia hospitali hiyo ya Bugando imeanza kutoa huduma ya mionzi na kusafisha figo hivyo wanawataka wakazi wa Mwanza kufika hospitalini hapo na kuacha kwenda Dar es Salaam kufuata huduma hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Bima Bugando, Kelebe Luteli anasema hospitali hiyo imefanya maboresho makubwa kwenye Idara ya dharura inayoongozwa na madaktari bingwa watatu.

Anasema maboresho mengine yamefanyika katika vyumba vya upasuaji ambao vimeongezwa na kufikia 12 kutoka vitano vilivyokuwapo hapo awali.

"Kwenye hivyo vyumba tumeweka vifaa vya kisasa na ukarabati huo mzima pamoja na ujenzi wa vyumba vipya umegharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni mbili, baada ya kuongeza vyumba hivi wananchi sasa wanafanyiwa upasuaji ndani ya siku tatu," anasema

No comments:

Post a Comment

Pages