MAMLAKA ya
Elimu na Mafunzo ya Fundi Stadi (VETA), imesema kuwa imejipanga
kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 740,000 hadi kufikia 1,000,000
ifikapo 2021/22.
Pia VETA imewaalika wananchi kutembelea banda lao lililopo katika viwanja vya maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam 'Sabasaba', ili kujionea teknolojia mbalimbali.
Hayo
yameelezwa na Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Sitta Peter alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika
viwanja vya maonesho hayo.
Amesema VETA imejipanga kuwajengea uwezo vijana wawe na ubunifu wenye umahiri wa kubuni vitu mbalimbali kwa mahitaji ya jamii.
"Hii
yote tunaonesha ni kwa namna gani tunachangia katika sekta ya viwanda,
kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha ulioisha kulikuwa na miradi 40 ya
ujenzi na upanuzi wa vyuo. Katika hiyo miradi inahusisha pia vyuo vipya
25 vya Wilaya ambavyo tunavijenga kwa nguvu za ndani," amesema.
Ameongeza
kuwa, pamoja na miradi hiyo, pia wana miradi mingine 10 ya Halmashauri
na hivi karibuni wamezindua vyuo vitatu katika Halmashauri ya Ileje,
Nkasi na Nyamidaho.
Akizungumzia
kuhusu maonesho hayo, amesema kuwa kwa mwaka huu wamefanikiwa kuja na
teknolojia 12 mpya zikiwamo mashine ya ubuyu, kuchemsha maji pasipo
kutumia umeme, mfumo wa kunawa maji bila koki, kuingiza umeme mita ukiwa
mbali, ushonaji wa kidigitali, mashine ya kupanda mazao, ukaushaji bora
mazao ya Samaki na nishati ya umeme pasipo chanzo cha mafuta wala
maji.
Pia teknolojia
nyingine ni teknolojia ya kuchenjua madini kutoka kwenye madini pasipo
kutumia zebaki, ubunifu wa samaki kikiwamo kitanda tiba na kochi.
No comments:
Post a Comment