Bwawa
la Kidete lililolalamikiwa na wananchi wa Kilosa Mkoani Morogoro wakati
wa ziara ya Rais Dkt Magufuli Wilayani humo limebainika kusababisha
maafa ya watu 17 kwa mwaka huu pekee huku yakikata huduma ya maji safi
ya kunywa pamoja na kuharibu na kusomba mazao ya wananchi wa eneo hilo
la Kidete na kusababisha mafuriko katika mji wa Kilosa.
Adha
hiyo imebainika baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
John Pombe Magufuli kupokea malalamiko ya wananchi na kuagiza viongozi
wa serikali kufika eneo hilo la Kidete na kujionea athari
zinazolalamikiwa ambapo wananchi hao wamesema Bwawa la Kidete limegeuka
kuwa kero badala ya fursa baada ya kingo za Bwawa hilo kuharibika
Mara
baada ya wananchi hao kutoa malalamiko yao, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi
aliyeambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba kwa lengo la
kutekeleza agizo la Rais, amesema malalamiko ya wananchi wa Kidete ni
dhahiri na yana mashiko baada ya kujionea mwenyewe na kuwaomba wananchi
hao kuwa na subira wakati serikali ikiangalia utaratibu wa kutatua kero
hiyo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, amesema ni kweli
Bwawa hilo kingo zake zimebomoka na kusababisha maafa na kuwataka
wananchi hao kuitumia changamoto hiyo kama fursa pale Bwawa hilo
litakapojengwa upya ili liweze kutumika kwa shughuli nyingine za
uzalishaji kama vile uvuvi na kilimo cha umwagiliaji
Bwawa
la Kidete lilijengwa na wakoloni wa kijerumani wakati wa ujenzi wa reli
ya kati kwa lengo la kupunguza mafuriko kutoharibu miundo mbinu ya reli
hiyo na kuharibika miaka ya 1990 na tangu wakati huo halijafanyiwa
ukarabati jambo ambalo limesababisha maafa na adha kwa wananchi wa eneo
la Kidete Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro hadi pale wananchi hao
walipolalamika kwa Rais Dkt Magufuli na kuagiza ufuatiliaji wa kero hiyo
ufanyike.
No comments:
Post a Comment