Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama maziwa yanayotokana na korosho
wakati alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Naliendele, Mtwara,
Julai 7, 2020. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk. Fortunus Kapinga (kushoto),
kuhusu utafiti wa mbegu bora za mhogo unaofanyika katika Taasisi hiyo,
Julai 7, 2020. Wa pili kushoto ni Mtafiti Mkuu katikaTaasisi hiyo,
Bernadetha Kimata. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli itahakikisha kwamba vyuo na vituo vyote vya utafiti wa kilimo nchini
vinafufuliwa, hivyo Wizara ya Kilimo inatakiwa kutenga fedha za kutosha katika
bajeti yake kila mwaka.
“Nataka niwahakikishie
Serikali yenu imedhamiria kuimarisha kilimo pamoja na utafiti wake. Mwezi mmoja
uliopita nilikuwa Mlingano mkoani Tanga kuona shughuli za utafiti wa zao la
mkonge lakini miezi miwili iliyopita nilikuwa kwenye chuo kipya
tulichokianzisha kule Kigoma cha utafiti cha Kihinga na nimeona kazi yake na
tutapata mafanikio makubwa.”
Waziri Mkuu alitoa kauli
hiyo jana (Jumanne, Julai 07, 2020) alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Naliendele iliyoko mkoani Mtwara kwa lengo la kujionea shughuli za utafiti wa
mazao mbalimbali ya kilimo zinazoendelea kituoni hapo.
Alisema Rais Dkt. John
Pombe Magufuli amefurahishwa na kazi nzuri za utafiti wa mazao mbalimbali
zinazofanywa na vituo vya utafiti na matokeo mazuri ya utafiti huo kwa wakulima
wa Watanzania.
Waziri Mkuu alisema “Azma
ya kusimamia na kuona vyuo vya utafiti vinafanya kazi yake vizuri ni pamoja na
maboresho haya kwanza wizara husika lazima itambue kuwa vyuo vya utafiti vinamchango mkubwa,
wizara kwenye bajeti zake ipeleke fedha nyingi kwenye utafiti na tuone utafiti
unagundua mambo na yale yanayogunduliwa yaende yakafanyiwe kazi.”
Vilevile, Waziri Mkuu
alisema idadi ya udahili wa wanafunzi katika vyuo vya kilimo itaongezwa ili
wapatikane wataalamu na watafiti wengi ambao wanahitajika sana katika
kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini.
Tasisi ya hiyo ya Kilimo
ya Naliendele ni miongoni mwa vituo vya utafiti wa kilimo nchini ambavyo
vimewawezesha wakulima wengi kujiongezea tija na kujikwamua kiuchumi baada ya
kutumia mbegu bora zinazozalishwa kituoni hapo kama za korosho, ufuta na
muhogo.
No comments:
Post a Comment