Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Na Mwandishi Wetu
CHAMA
Cha ACT-Wazalendo leo kimetambulisha rasmi viongozi wa timu ya kampeni
ya kitaifa kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28/2020.
Timu
hiyo ya ushindi imetambulishwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe
leo Agosti 18, 2020 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.
Katika
kikao chake na waandishi wa habari katika Ofisi za chama, Magomeni Dar
es Salaam, Zitto aliwataja wajumbe wa timu hiyo ni Mwenyekiti wa Timu
ya kampeni ya ACT–Wazalendo kuwa ni Joram Bashange ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Wakili Emmanuel Lazarus Mvula ambaye atakuwa Meneja wa kampeni Taifa.
Pia katika mkutano huo na waandishi wa habari, kiongozi wa chama amezungumzia matukio ya utekwaji, kupigwa
na kujeruhiwa kwa wanachama na wagombea waliotia nia katika nafasi ya
ubunge na udiwani ndani ya chama cha ACT- Wazalendo katika Jimbo la
Ruangwa mkoani LIndi.
Aliwataja wahanga wa matukio hayo kuwa ni Said Ally Nangendekwa ambaye alipigwa na kujeruhiwa nyumbani kwake Agosti 9 2020.
"Mwingine ni Joakim Ng’ombo ambaye alitekwa, kupigwa Agosti 12 na kuokotwa wilayani Mkuranga mkoani
Pwani
Agosti 13 akiwa na hali mbaya ambapo awali alitibiwa katika Hospitali
ya Temeke na sasa amehamishiwa Hosptali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya zaidi.
Mtu
wa tatu ni Bakari Abdallah Nanyambo ambaye ni mgombea udiwani wa ACT-
Wazalendo alishambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana ambapo hivi
sasa anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Mbekenyera mkoani
Lindi," alisema.
Alisema matukio haya yote yameripotiwa katika vituo vya polisi mkoani humo.
Zitto
alisema kutokana na matukio hayo, anaomba yafuatayo yazingatiwe: Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ifuatilie kwa karibu na kutolea ufafanuzi
matukio haya kama ni ya kisiasa basi ikemee na kuchukua hatua.
Aidha, amewataka wanachama wa ACT- Wazalendo wachukue hatua za kujilinda, kulinda viongozi wao na mali za
chama.
"Chama
kinawaagiza wanachama wote kufuata taratibu za kisheria wakati wote
kuelekea Uchaguzi Mkuu na pale wanapoona haki zao au haki za wengine
zinavunjwa watetee na kuzuia uvunjwaji wa haki kwa kuripoti matukio hayo mahali panapohusika," alisema.
No comments:
Post a Comment