Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilakala Moshi Kahiki akizungumzia madhila wanayopitia kwa kijiji chao kukosa miradi ya Usimamizi Shirikishi ya Misitu ya Jamii (USMJ).
Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Ilakala wakiwa kwenye mkutano wa Halmashauri hiyo.
Na Suleiman Msuya
"TUNAUMIA
sana kuona wenzetu wa Kitunduweta, Ulaya Mbuyuni, Muhenda, Ihombwe na
kwingineko wanavyonufaika na misitu yao kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi
katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS)," hayo ni maneno ya Mwenyekiti wa
Kijiji cha Ilakala, kata ya Muhenda wilayani Kilosa mkoani Morogoro,
Moshi Kihiki.
Kihiki
alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo
mbalimbali vya habari ambao walitembelea vijiji vya Matuli wilayani
Morogoro, Msolokelo Mvomero, Ulaya Mbuyuni na Kitunduweta Kilosa kuona
namna mradi wa TTCS ulivyobadilisha maisha ya wanavijiji kiuchumi,
kijamii na maendeleo.
Mradi
wa TTCS unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA),
chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Mwenyekiti
huyo alisema wanaumia katika mtazamo wa wivu kutokana na ukweli kuwa
majirani zao wamefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo hali
ambayo kwao ni kinyume.
Alisema
wanakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii, kiuchumi na maendeleo
huku wakiwa na rasilimali misitu mingi ila wameshindwa kuitumia kama
wenzao ambao wapo mradi wa TTCS.
"Tuseme
kweli tunaumia kwa wivu kwani wenzetu wanatatua changamoto zao kama
ujenzi wa shule, zahanati, maji na nyingine muhimu kwa kutumia fedha
zinazotokana na Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) baada ya
kupata elimu kupitia TTCS," alisema.
Alisema
kwa sasa wanahitaji kupata mradi wa TTCS ili nao waweze kunufaika na
rasilimali misitu iliyopo kijijini kwao kwani kwa sasa amepata elimu na
kutambua faida wanazopata vijiji jirani.
Kihiki
alisema kwa sasa wanatekeleza miradi ya maendeleo kupitia ruzuku ya
halmashauri ambayo haitoshi kutatua changamoto zao hivyo kupelekea
kuchangisha wanakijiji jambo ambalo kwa wenzao halipo.
Naye
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Ilakala, Inviolata Mvura aliomba TFCG
na MJUMITA kuwapelekea mradi wa TTCS kwa kuwa wapo tayari kuuendeleza
kama walivyo majira zao.
Mjumbe huyo alisema misitu waliyonayo inatumika bila utaratibu hali ambayo inazidi kuwarejesha nyuma kimaendeleo.
"Sisi
hapa Ilakala tuna misitu mingi ya asili lakini inatumiwa vibaya kwa
watu kuanzisha mashamba na mifugo kuingia. Naomba nitumie nafasi hii
kuwakaribisha TFCG na MJUMITA ili na sisi tupunguze maumivu ambayo
tunapitia kwa sasa," alisema.
Mvura alisema iwapo watapata elimu ya kutumia msiitu kwa njia endelevu wataweza kufikia maendeleo ambayo wenzao wamefikia.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Serikali Kijiji, Zuberi Kiokoteke, alisema
kijiji chao bado kipo nyuma kimaendeleo hivyo wanaamini mradi wa TTCS
ukija kwao watapata maendeleo.
Alisema
shule ya Msingi Nyaranda ambayo ipo kijijini hapo ina hali mbaya hivyo
wanaamini kuwa wakiwa katika mipango ya TFCG na MJUMITA wataibadilisha
kuwa ya kisasa.
Ofisa
Maliasili wa Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo alisema wilaya hiyo ipo
katika mkakati wa kusambaza dhana ya USMJ katika vijiji vyote vyenye
misitu ya asili na Ilakala kinaweza kuwa kimojawapo.
"Sisi
halmashauri tunajua faida ya USMJ hivyo tunajipanga kwenda katika
vijiji vingine venye misitu ya vijiji kuwapatia elimu kuhusu uhifadhi
lengo likiwa ni kuwa na jamii inayotambua faida za misitu," alisema.
Mtimbanjayo
alisema mradi wa TTCS kwa kipindi cha miaka saba ya kuwepo Kilosa
umefanikiwa kuingizia vijiji takribani 16 kati ya 20 zaidi ya shilingi
bilioni ambapo halmashauri imepata takribani shilingi milioni 100.
Ofisa
Sera na Majadiliano wa MJUMITA, Elida Fundi alisema wameamua
kuwapitisha waandishi wa habari katika vijiji ambavyo havina mradi ili
wasikie kilio cha wanavijiji hao.
Fundi
alisema mwamko wa vijiji kutekeza USMJ ni mkubwa hivyo ni jukumu la
Serikali kupitia halmashauri yake kutekeleza kwa vitendo USMJ kwa kuwa
ina manufaa chanya.
"Nadhani
mmesikia kilio cha wanavijiji wenye misitu ya asili ni kupewa elimu
namna ya kuitumia misitu kwa njia endelevu kama wanavyofanya wenzao wa
vijiji 20 hapa Kilosa," alisema.
Ofisa
huyo alisema iwapo vijiji vyote vyenye misitu ya asili ambayo inaweza
kutumika na kujizaa upya vingeweza kuwekeza katika dhana ya TTCS ni wazi
kuwa wanavijiji wengi watanufaika.
No comments:
Post a Comment