Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehama Bwasi (kulia) akipokea majarida yanayohusu shughuli mbalimbali za mradi zinazofanywa na Shirika la Usimamizi wa Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) kutoka kwa Ofisa Uhusiano wa shirika hilo Bettie Luwuge(kushoto) baada ya kufika ofisini kwa Mkurugenzi huyo.
Baadhi
ya wananchi wa Kijiji cha Matuli wakiwa kwenye kikao cha kujadili
mafanikio na changamoto za mradi wa mkaa endelevu kwenye kijiji chao.
MKURUGENZI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi, amesema kutokana na
fursa zilizopo katika Usimamizi wa Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ)
wameamua kussambaza fursa hiyo katika vijiji vipya vitano.
Bwasi
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao
wapo katika ziara ya kuangalia faida na changamoto zilizopo kwenye
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), ambao
umetekelezwa kwenye vijiji vitano vya halmashauri hiyo.
Alisema
mradi wa TTCS umeonesha matokeo chanya katika vijiji vitano vya Matuli,
Diguzi, Lilongwe, Mlilingwa na Tununguo hivyo katika bajeti ya
2020/2021 wataanza kutekeleza vijiji vipya vitano.
"Mafanikio
ambayo tumeyapata kwenye vijiji vitano vya awali tunataka tuhamishie
kwa vijiji vipya vya Rumba Chini, Sesemba, Kiropa na Pangawe ambapo
kuna misitu ya asili," alisema.
Alisema
dhamira yao ni kuona wananchi wanapata maendeleo kupitia rasilimali zao
na misitu imeonesha matokeo chanya kwa wananchi wengi wenye misitu.
"Kutokana
na maendeleo ambayo wilaya pamoja na wananchi hao imeyapata kutokana na
mradi huu, mkakati uliopo ni kuwepo kwa mradi wa aina hiyo katika
vijiji vingine hasa kwa kuzingatia Wilaya ya Morogoro imejaaliwa kuwa na
eneo kubwa la misitu ya asili," alisisitiza.
Mkurugenzi
huyo alisema USMJ imechochewa na Shirika la Kuhifadhi wa Misitu ya
Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA), kupitia TTCS hivyo wanaamini kuanzisha vijiji vipya
ni uamuzi wa kuwaunga mkono wadau.
"Kama
mnavyofahamu halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro imebarikiwa kuwa na
misitu mingi ya asili , na misitu hii kwa kiasi kikubwa iko chini ya
uhifadhi lakini vile vile inamilikiwa na vijiji, kwa hiyo nichukue fursa
hii kushukuru TFCG na MJUMITA, wameweza kushirikiana na halmashauri
yetu na vijiji vyetu vitano.
"Katika
kuimarisha na kuzalisha mkaa asili kama tunavyofahamu shirika hili
uwepo wake katika halmashauri yetu umeweza kutengeneza tija kubwa kwa
halmashauri na wananchi wa vijiji ambavyo vinafanya kazi na shirika
hili," alisema.
Alisema
mbali na uhifadhi wa asili kama shirika lenyewe dhima yake, lakini uwepo
wa shughuli hiyo ya mkaa endelevu katika halmashauri yetu kumeleta
maendeleo makubwa kwa wananchi wetu.
"Kwa
kweli haijawahi kutokea kuwepo na mkaa endelevu katika halmashauri
yetu, vijiji hivyo vitano vimeweza kujipatia fedha nyingi sana, kwa
mfano kijiji kimoja kimepata zaidi ya shilingi milioni 100, ni kitu
ambacho kwa kweli hakijawahi kutokea miaka yote ya nyuma.
Kuwepo
na shughuli ya uzalishaji mkaa endelevu kumepanua wigo mkubwa, kwanza
kujikusanyia mapato ya kutosha, ambapo mapato hayo yapo chini ya vijiji
ambavyo vinatekeleza mradi huo," aliongeza.
Pia
alisema kumekuwepo na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umesaidia
kutengeneza wigo wa kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Kwa
upande wake Ofisa Maliasili wa wilaya hiyo Waida Salim, alisema mradi
wa TTCS, umeleta mapinduzi maakubwa katika vijiji husika hivyo baada ya
kutoa elimu zaidi vijiji vingine vipya vimeonesha uhitaji.
Salim
alisema rasilimali misitu ikitumiwa katika mipango sahihi inauwezo wa
kubadilisha maisha ya jamii husika huku uhifadhi ukiimarika zaidi.
"Misitu
ni uhai na maendeleo iwapo jamii itaamua kuitumia vizuri na hapa kwetu
tumethubutu na tumeweza sasa ni wakati wa kuhamishia mafanikio haya na
matunda yanaonekana Matuli, Mlilingwa, Diguzi na kwingineko," alisema.
Naye
Sadiki Kondo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili katika
Kijiji cha Matuli, alisema USMJ ni fursa ambayo ilijificha kwa muda
mrefu hivyo wanaitumia vizuri kuchochea maendeleo.
Alisema wananchi wa kijiji chao kwa sasa ni walinzi wa rasilimali misitu kutokana na manufaa ambayo yametokana na USMJ.
No comments:
Post a Comment