Na Janeth Jovin
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga, Septemba 7, mwaka huu kusikiliza utetezi katika kesi ya uchochezi, inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo leo lakini ilishindwa kuendelea baada ya mawakili wa utetezi kushindwa kufika mahakamani hapo.
Mdee amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa mawakili wake, Peter Kibatala na Hekima Mwasipu, wameshindwa kufika mahakamani hapo kwa sababu wapo kwenye kesi nyingine katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara na Kazi.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya mshitakiwa kuanza kujitetea.
Simon amedai kuwa kutokana na mawakili wa mshitakiwa huyo kutokuwepo mahakamani hapo, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya utetezi.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, 2020 kwa utetezi.
Mdee anadaiwa kuwa Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, alitenda kosa la kutoa lugha chafu.
Anadaiwa alitamka maneno machafu dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea hovyo hovyo , anatakiwa afungwe breki” na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
No comments:
Post a Comment