Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT, Profesa Zacharia Mganilwa akiangalia Reli ya Kisasa (SGR) inayojenga hivi sasa.
Na Janeth Jovin
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana na Serikali kimesema kuwa kitahakikisha nchi inapata wataalamu wengi wazawa ambao kwa miaka mitano ijayo ndio watakaojenga reli za kisasa na madaraja makubwa hapa nchini.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa wakati wa ziara ya viongozi wa baraza la chuo hicho ambao walitembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliyowafikisha hadi kwenye handaki la kupitia treni ya kisasa lenye urefu wa Kilomita 1.003 sawa na Mita 1131 lililopo eneo la Mkadage Wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Profesa Mganilwa amesema taifa la Tanzania tayari limeshafikia katika uchumi wa kati hivyo ni muhimu kuwepo kwa wataalamu wa kutosha ambao watakaoweza kujenga miundombinu ya reli ya kisasa na barabara hivyo kuwafanya abiria kufika kwa wakati sehemu mbalimbali.
Aidha amesema lengo la ziara waliyoifanya katika Shirika la Reli Tanzania (TRC) ni kwenda kuangalia changamoto iliyopo upande wa wasilimali watu katika mradi wa SGR na kuongeza kwa sasa nchi bado inakabiliwa na upungufu wa wataalamu kwenye masuala ya reli
"Sasa hivi ndio tunaelekea kuzalisha wataalamu hivyo wakiwepo kwa wingi wale wenye sifa hasa katika sekta ya reli, bandari na viwanja vya ndege wataweza kuajiliwa na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa," amesema Profesa Mganilwa na kuongeza
"Kazi zitakapotangazwa wakandarasi wa kitanzania wataweza kushindana na wale wa nje na utafika wakati tunaweza tusiwe kabisa na wakandarasi kutoka nje kuja kuchukua miradi mikubwa ya hapa nchini," amesema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema anaishukuru bodi ya NIT kwa kutembelea shirika hilo na kuongeza kuwa wataalamu wengi upande wa usafirishaji waliopo TRC wametokea katika chuo hicho.
Amesema NIT ni chuo muhimu katika Shirika lao kwani zaidi ya Trilioni saba zimewekezwa katika mradi wa SGR hivyo ni muhimu nchi kuwa na vyuo vitakavyozalisha wataalamu watakwenda kusimamia miradi hiyo na sekta ya usafirishaji kwa ujumla.
"Ili tupate wataalamu hao lazima tuwe na chuo na kilichopo ndo hichi cha NIT, ujio wao hapa kwenu ni wa manufaa makubwa na ninaamini ushirikiano huu utaendelea," amesema Kadogosa
Meneja Msaidizi wa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, Ayoub Mdachi amesema kwa sasa ujenzi wa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 87 huku kipande cha Morogoro hadi Makotopola ukifikia asilimia 35.
Aidha Mdachi amesema NIT wametembelea mradi wa SGR ili kuangia namna ambavyo TRC wanasimamia mradi huo mkubwa wa Taifa ili na wao kama chuo waweze kufanya maamuzi ya kusaidia Serikali katika kufundisha na kutoa wataalamu wa kutosha kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake Mtaalamu na msimamizi wa ujenzi wa mahandaki ya reli katika mradi wa SGR, Amili Hamis amesema mradi huo jumla ya mahandaki manne yenye jumla ya urefu wa mita 2620.
Amesema kwa hivi sasa maendeleo ya mahandaki hayo ni mazuri kwani yote yameshamalizika kuchimbwa na kazi iliyobaki ni kuyajengea zege juu ambapo handaki la pili limeshakamilika kwa asilimia 100.
"Handaki la pili limeshakamilika kilichobakia ni uwekaji wa kokoto, reli na umeme, katika handaki la kwanza ambalo limefikia asilimia 98 tunamalizia kutengeneza njia za wapitao kwa miguu na kuweka umeme, handaki la tatu tumemaliza uchimbaji sehemu ya juu na la nne nalo limeshachimbwa na tumemwaga zege za chini na kazi ya Kuweka nondo kwa ajili ya kumwaga zege la juu inaendelea," amesema
No comments:
Post a Comment