Magari ya mizigo yakipita katika moja ya vipande vinavyokarabatiwa katika barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92) ambapo ukarabati wake unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. PICHA NA WUUM.
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Masiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, ametoa siku Tatu kwa Uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kagera kuhakikisha wanakamilisha ukarabati wa barabara ya Rusumo - Lusahunga (KM 92) ambayo imekuwa kero kubwa kwa wasafirishaji wa mizigo ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa ukagauzi wa barabara hiyo, mkoani Kagera, Mwakalinga, amemtaka Kaimu Meneja wa Mkoa huyo na wasaidizi wake kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kuanzia leo ili kuruhusu magari ambayo yameshindwa kupita kuendelea na safari zake kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
“Nadhani Meneja umenielewa, nataka ndani ya siku Tatu kama ulivyoahidi barabara hii iwe inapitika, na hakikisheni mnafanya kazi usiku na mchana kuanzia leo ili mkamilishe kazi hii”, amesema Mwakalinga.
Aidha, Mwakalinga ameongeza kuwa barabara hiyo inatakiwa kuwa yenye viwango bora kutokana na umuhimu wake katika uchumi wa nchi, na hivyo kumuelekeza Mkurugenzi wa barabara wa Sekta hiyo Mhandisi Hussein Mativila, kuhakikisha wanatazama kwa jicho la pekee na kuzipa kipaumbele barabara zote ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi jirani.
Mwakalinga, amefafanua kuwa barabara hiyo imetengewa kiasi cha shilingi Bilioni 12.5 ambazo ni kwa ajili ya kuwekewa lami ambapo kwa kuanza ameelekeza utekelezaji wa fedha hizo uanze kwa kurekebisha vipande vilivyoharibika sana.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Jackson Lwerengera, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kukamilisha ukarabati wa barabara hiyo ndani ya siku alizowaagiza.
Amesema kuwa TANROADS Mkoa huo ulitekeleza kazi za dharura chini ya matengenezo ya muda maalumu katika barabara hiyo ambapo kilometa 6.7 kwa sehemu ya Kwanza na Kilometa 7.1 za sehemu ya pili zimekamilika.
Mhandisi Lwerengera, ameeleza baadhi ya changamoto kuwa barabara hiyo kuchelewa kufanyiwa matengenezo makubwa kutokana na ongezeko kubwa la magari ambalo linahitaji tabaka la zege ya lami badala ya lami nyepesi ambayo ndiyo iliyopo na inayotumika kwa marekebisho ya sasa.
Barabara hiyo ambayo ina historia ya miaka 35 tangu ilipojengwa imekuwa ni kiungo kikubwa katika masuala ya kiuchumi kati ya nchi yetu na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Congo (DRC) kutokana na wafanya biashara wengi kutumia barabara hiyo kusafirisha mizigo yao.
No comments:
Post a Comment