HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 27, 2020

WARASIMISHAJI ARDHI ARUSHA WATAKIWA KUKAMILISHA IFIKAPO AGOSTI 30


Kiongozi wa kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi cha kutatua changamoto za urasimishaji PrayGod Shayo (aliyeshika kamba) akiongoza ukaguzi wa uwekaji alama za upimaji katika maeneo ya hifadhi ya bararabara ya Arusha -Moshi katika Kata ya Matevesi mkoani Arusha. 

 

 Na Mwandishi Wetu

 
URASIMISHAJI makazi ni fursa  yenye lengo la  kuinua uchumi wa mwananchi mmojammoja  wa hali ya chini na Taifa kwa ujumla.
 

Hayo yamebainishwa  mkoani Arusha na Mratibu wa kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kilichoundwa kwa ajili ya kutatua na kukwamua changamoto za urasimishaji makazi holela PrayGod Shayo, katika ukaguzi unaondelea kwenye mitaa mbalimbali ya Mkoa humo ambapo zoezi la kurasimisha makazi linaendeshwa na makampuni
ya watu binafsi.

Akizungumza na kamati ya urasimishaji katika mtaa wa Kambi ya Maziwa, Kata ya Matevesi Shao alisema, urasimishaji una faida kubwa kwa mwananchi mmoja mmoja lakini pia kwa Taifa nzima. 

Kazi kubwa ya warasimishaji na kamati walizo nazo pamoja na kusimamia mikataba ya urasimishaji ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa urasimishaji makazi.
 

Aliongeza kwamba, katika kuelekea uchumi wa kati, wananchi wanatakiwa kuishi katika maeneo ambayo yamepangwa na kupimwa ili waweze kupata huduma za msingi za kijamii. Upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo yanayo wazunguka wananchi ni fursa kwao kiuchumi.


“Kama maeneo yakiwa yamepangika na kupimwa vizuri kwenye mitaa, lazima wananchi watakuwa wanafanya biashara ndogondogo na kujipatia kipato, pia watakuwa na barabara za kupitisha bidhaa zao endapo watahitaji kuzisafirisha kutoka mtaa mmoja kwenda mtaa mwingine,“alisema Shao.


Aidha, Rubeni Mpanda katibu wa kamati ya urasimishaji mtaa wa Kambi ya Maziwa alisema, zoezi linaenda vizuri na wananchi wanashirikishwa japo changamoto ni kwamba baadhi yao hawapatikani kwenye makazi yao wakati wa utekelezaji na hivyo kulazimisha kazi kufanyika polepole.


Mpanda aliongeza kwamba, yeye na viongozi wenzake wa kamati ya urasimishaji walishawatembelea wananchi wote ambao bado hawajawekewa alama za upimaji (beacons) na kuwaomba angalau siku za Jumamosi na Jumapili washirikiane na warasimishaji ili kuwawekea alama za upimaji katika maeneo yao lakini hawajafanikiwa bado.


‘Urasimishaji ni lazima uwe zoezi shirikishi ndiyo maana kazi
inafanyika taratibu ili kila mwananchi aridhike na ashiriki katika zoezi la uwekaji alama za upimaji. Malalamiko mengi yaliyopo ya urasimishaji ni kutoka kwa wale ambao tunawafuatilia na hawapatikani kwa sababu mwisho wa siku ni lazima kazi iendelee,“alisema Mpanda.
 

Siku zote wananchi wanaamini ahadi wanazopewa awali katika utambulisho wa mradi. 

Matumaini mengi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha yalikuwa kuona mradi wa urasimishaji unatekelezeka kwa wakati.


Kuchelewesha utekelezaji kunasababisha maswali na hofu kwa wananchi ambao walishachangia fedha zao kwenye huo mradi.

 Warasimishaji wote katika mkoa wa Arusha wamepewa hadi Agosti 30, mwaka huu 2020 wakamilishe kazi zote za urasimishaji ili wananchi waweze kuandaliwa hati za umiliki katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

Pages