HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 30, 2020

DK. Kijaji aahidi makubwa kwa wananchi wa Kondoa

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ashatu Kijaji, amewaomba wananchi wote wa jimbo hilo kumchagua  yeye pamoja na  mgombea wa urais kupitia chama hicho Dk. John Magufuli ili wakashirikiane tena kuwaletea wananchi maendeleo.


Akizungumza wakati wa muendelezo wa kampeni zake alizofanya katika vijiji vya Makafa, Kwadelo, Kwachuli na Lembo vilivyopo katika Kata ya Salanka Dk Kijaju alisema endapo atachaguliwa  atahakikisha anaipaisha Kondoa kimaendeleo kama ambavyo ilani ya CCM ilivyokusudia kufanya hivyo nchi nzima.

Alisema kwa kushirikiana na Serikali, atasimamia masuala yote muhimu na yenye tija kwa wananchi wa jimbo hilo  kwa kuboresha huduma za afya, elimu ili kuwawezesha watoto wote kufanya vizuri katika mitihani yao na kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu.


"Serikali ya CCM chini ya Dkt Magufuli imefanya mazuri kwenye Sekta zote nawaahidi kuwa tutalimaliza tatizo la maji kwenye vijiji vya Jimbo letu baada ya mafanikio makubwa ya kuchimba visima virefu  vya maji 64 kwa miaka mitani ya uongozi wetu"alisema Dk Kijijaji.

Dk Kijaji ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, alisema mikakati yake  mingine endapo atapewa ridhaa hiyo na wananchi ni pamoja na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo hilo, jambo ambalo lililosisitizwa pia katika ilani ya chama hicho.

"Nawombeni wananchi  wote mkafanye maamuzi sahihi siku ya Oktoba 28 kwa kunipiga kura mimi, Mheshimiwa Dk John Magufuli kwa nafasi ya Urais, wagombea wote wa udiwani wa Chama cha Mapinduzi ili tuendelee na mikakati yetu ya kuwaletea maendeleo" alisema Dk Kijaji

Aidha alisema Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) imefanya mambo mengi na makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya utawala wa Rais Magufuli ikiwemo ujenzi wa miundombinu  ya Barabara, madaraja, Reli ya kisasa ya 'SGR' na Bwawa la kufua umeme la Nyerere lakini pia ununuzi wa ndege, jambo lililoifanya Tanzania kuzidi kusonga mbele.

Amewaomba kupikigia kura chama hicho ili pamoja na mambo mengine Rais, wabunge na madiwani wote kupitia chama hicho waweze kushirikiana kwa lengo la kufanikisha maendeleo zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

No comments:

Post a Comment

Pages