HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 30, 2020

KESI YA IDRISS SULTAN YAAHIRISHWA

KESI ya kuchapisha maudhui mtandaoni bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inayomkabili Msanii wa Vichekesho, Idriss Sultan (27) na wenzake imeshindwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka, kwa sababu Wakili wao hakuwepo Mahakamani.


Mbali na Sultan washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Dokta  Ulimwengu (28) Mkazi wa Msasani na Isihaka Mwinyimvua (22) Msanii na Mkazi wa Gongo la Mboto.

Wakili wa Serikali, Adolf Ulaya amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka.

Baada ya Wakili Ulaya kudai hayo, Idriss aliieleza mahakama kuwa wakili wao, Elia Ryoba ana hudhuru, kwa hiyo wanaomba Mahakama ipange tarehe nyingine ambayo Wakili wao atakuwepo.

Hakimu Ruboroga, baada ya kuwasikiliza, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 29, 2020 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Katika mashtaka yao, Wakili  Ulaya alidai kuwa washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8,2016 na Machi 12,2020 maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Alidai washitakiwa hao walichapisha maudhui kupitia chaneli ya Local Motion ya YouTube bila kuwa na leseni ya TCRA.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana.

Hakimu Ruboroga alimtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kila mmoja.

Washitakiwa wote walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

No comments:

Post a Comment

Pages