Na Irene Mark
WAKAZI wa mikoa 11 inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, wameshauriwa kuchukua tahadhari ya mvua za wastani na juu ya wastani zitakazoanza kuonyesha wiki ya pili ya Novemba,2020.
Mvua hizo zitaendelea kuonyesha kwa vipindi tofauti hadi wiki ya mwisho ya Aprili, 2021.
Akitangaza utabiri wa msimu kwa maeneo ya nchi yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, ofisini kwake Dar es Salaam leo Oktoba 21,2020. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, alizitaka mamlaka na wananchi kutopuuza taarifa za hali ya hewa.
Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) aliisisitiza jamii na mamlaka husika kuzingatia na kuchukua tahadhari ya taarifa za TMA.
Akiitaja mikoa itakayopata mvua hizo, Dk. Kijazi alisema ni Singida na Dodoma iliyopo Kanda ya Kati na Mtwara, Lindi na Ruvuma inayopatikana kwenye Pwani ya Kusini na Kusini mwa nchi.
Mikoa mingine ni Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe na Kusini mwa Morogoro iliyopo Nyanda za Juu Kusini Magharibi,
Hata hivyo aliitaja mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi kwamba itapata mvua za wastani na chini ya wastani hivyo watumie vizuri maji na kupata ushauri wa wataalam kuhusu mbegu za mazao yanayostahimili ukame.
Kwa mujibu wa Dk. Kijazi, kipindi hicho cha mvua za msimu hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
"Wakulima watarajie unyevu wa kutosha unaoweza kuathiri mazao yao wasiopata ushauri wa kitaalam maana unaweza kuwa unyevunyevu uliopitiliza utakaoleta mmomonyoko wa udongo, kupotea kwa rutuba na kutuama kwa maji mashambani.
"Tunashauri matumizi sahihi ya rasilimali maji kwa ajili ya uchakataji wa madini, uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani na majumbani kutokana na ongezeko la kina cha maji kwenye mabwawa na mtiririko wa maji kwenye mito," alisema Dk. Kijazi.
Aliongeza kuwa katika msimu huo kunaweza kutokea uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyoweza kujitokeza.
Hivyo, aliiasa jamii kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi katika vipindi vya ukavu vinavyoweza kujitokeza, pia kuhifadhi unyevunyevu wa udongo katika maeneo yatakayopata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mkurugenzi huyo alizishauri mamlaka za usafirishaji kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchukua tahadhari stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.
"Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko hivyo, kuharibu miundombinu, upotevu wa mali na maisha ya watu... ndio maana tunawataka wananchi na mamlaka husika kuboresha mifumo ya kupitishia maji taka na kuisimamia ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mafuriko," alisisitiza Dk. Kijazi.
Kuhusu mifugo, uvuvi na utalii, Dk. Kijazi alisema hali ya malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi.
" Hiki ni kipindi ambacho magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza kutokana na vipindi vya mvua nyingi kama vile homa ya bonde la ufa, kuoza kwa kwato na magonjwa ya minyoo kwa wanyama," alisema.
TMA imeshauri mamlaka za utalii kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na maji ili kuimarisha shughuli za utalii na menejimenti za maafa zimetakiwa kuchukua hatua stahiki ili kuzuia athari za mvua kubwa kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
No comments:
Post a Comment