HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 23, 2020

NHIF yateta na wahariri wa habari nchini



                                      
                                NA BETTY KANGONGA
 

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga amewaomba wahariri wa vyombo vya habari nchini, kuunga mkono agenda ya serikali kuwa na muswada wa kutungwa kwa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Konga alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa tano na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika jijini Dodoma ambapo walijadiliana na kushauriana masuala mbalimbali jinsi ya kuboresha huduma za mfuko huo ambao mwakani unaadhimisha miaka 20 tangu uanzishwe mwaka 2001.

Alisema vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha jamii, hivyo ni vyema kuwa na ushirikiano wa pamoja utakaohakikisha suala hilo linafanikiwa  ili watanzania wote wawe na Bima ya Afya itakayorahisisha upatikanaji wa matibabu.

"Wahariri mshiriki kutoa maoni na ushauri  wa kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na Umma kwa ujumla kwa kuwa ninyi ni mabalozi wa Mfuko," alisema. 

Konga alisema, kuwa wakati mfuko huo unaanzishwa ulihudumia watu wachache kutokana na baadhi kulalamikia huduma zilizokuwa zikitolewa.

Hata hivyo alisema maboresho makubwa yamefanyika sasa hasa katika  suala zima la upatikanaji wa dawa ambapo ndipo malalamiko yalikuwa kwa kiasi kikubwa.

"Tumepanua wigo wa upatikanaji wa dawa hasa kwenye upande wa vifurushi na tumefanikiwa kupunguza malalamiko ya wateja wetu," alisema.

Awali akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Idara Kuu ya Afya Bernard Mbanga alisema kuwa, hadi sasa jumla ya watu Milioni 4.4 pekee ndiyo wanaonufaika na huduma zinazotolewa na Mfuko huo.

Mbanga alisema kuwa Tanzania inajumla ya Watu Milioni 60 lakini wanufaika waliojiunga na huduma hiyo ni Milioni 4.4.

"Idadi hii kwetu bado ni ndogo kwani lengo letu ni kuhakikisha tunafanikiwa kwa kila Mtanzania kutumia huduma ya bima ya afya na kuachana na tabia ya kwenda kutibiwa kwa kutoa hela zao mifukoni, alisema na kuongeza kuwa 

...Serikali ipo katika majadiliano ya kuona asilimia 26 waliobaki na wasiokuwa na fedha ya kujiunga na mfuko ni namna gani itaweza kuwakomboa juu kupata huduma Bora ya afya." 

Alisema kwamba, serikali ipo katika harakati za kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages