Janeth Jovin
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Musoma, Mhe. John Rugalema Kahyoza amewataka Mahakimu wote
walioko katika Kanda ya Musoma kutumia taaluma yao kujibidisha kusoma
sheria na kuzitafsiri kwa umakini.
Akifungua mafunzo ya namna
bora ya uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo kwa Mahakimu 36
wa Kanda hiyo, Mhe. Jaji Kahyoza alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni
kutatua changamoto zilizojitokeza wakati alipofanya ukaguzi wa robo ya
tatu ya mwaka 2020 katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo zilizopo kwenye
kanda ya Musoma.
Aidha, Mafunzo hayo yalijikita katika taratibu
za uendeshaji wa mashauri ya mirathi, mashauri ya madai, mashauri ya
jinai, uandishi wa hukumu kwa Mahakama za Mwanzo na za Wilaya pamoja na
utekelezaji wa hukumu.
Katika mashauri ya mirathi, Mhe. Jaji
Kahyoza kwa kushirikiana na Mkaguzi wa Ndani wa Mahakama Kuu kanda ya
Musoma Bw. Andala Odock, waliwasisitiza Mahakimu hao kuzingatia taratibu
zote za msingi tangu kupokelewa kwa shauri la mirathi hadi kufungwa,
zikiwepo taratibu za kuthibitisha msimamizi wa mirathi, namna ya kutunza
wosia, kuzingatia mgawanyo wa mali kwa warithi, mchakato wa malipo, na
kufunga mirathi.
Jaji Kahyoza aliwasisitiza Mahakimu hao umuhimu
wa kufungua mashauri ya mirathi pale taratibu zote zinapokamilika pia
mashauri hayo yafunguliwe eneo analotoka marehemu kuepusha ufunguaji wa
shauri moja mara mbili.
Kwa upande wa mashauri ya madai na jinai,
Mhe, Kahyoza, aliwataka Mahakimu hao kuzingatia sheria na kuwa makini
katika kurekodi ushahidi unaotolewa mahakamani na hatua zote muhimu hadi
kufikia wakati wa kutoa hukumu. Pia aliwakumbusha taratibu za ukamataji
mali wakati wa kukaza hukumu.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Musoma, Mhe. Zephrine Galeba, alimpongeza Jaji
Mfawidhi kwa kuandaa mafunzo hayo elekezi ya kujengeana uwezo na
kukubali yafanyike kila robo mwaka kwani yatasaidia sana kuboresha
utendaji kazi hasa kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ambao huko ndiko
mashauri mengi yanaanzia.
Jaji Galeba pia aliwataka washiriki
wote kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi pamoja na sheria
ili kutoa maamuzi kwa uhuru jambo ambalo litalinda uhuru wa Mahakama.
No comments:
Post a Comment