HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 20, 2020

TAMBO NBC MARATHON

Na Mwandishi Wetu

JOTO la Mbio za Kimataifa za NBC Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 22 jijini Dodoma limezidi kupanda baada ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kuanza kuwasili jijini hapa huku wakimwaga tambo za kufanya vema.

Wanariadha kutoka Kenya tayari wameanza kuwasili jijini hapa huku kutoka Uganda wakitarajiwa kuwasili (leo Alhamis usiku), na wale kutoka Malawi wakitarajiwa kuwasili (kesho Ijumaa).

Mmoja wa wanariadha kutoka Kenya Joan Jerop Massah ametamba kufanya vema katika mbio za Kilomita 21 ‘Half Marathon’ na kuondoka na zawadi nono zilizoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Naye mwanariadha wa kike anayefanya vizuri katika mbio za Kilomita 42 ‘Full Marathon’ Sara Ramadhani kutoka Arusha amejinasibu kuhakikisha bendera ya Tanzania inang’ara na kukata ngebe za Wakenya.

Wanariadha wengine wa Tanzania walioahidi kufanya vema ni  pamoja na Hamis Misai, Jafar Rajab kutoka Singida waliojitosa Kilomita 42.

Shughuli pevu inatarajiwa kuwa kwenye Kilomita 21 ‘Half Marathon’ ambako wakali wengi wamejitosa.

Wanariadha nyota wa Tanzania waliojitosa katika mbio hizo ni pamoja na Mwanariadha wa kike ambaye tayari amefuzu kwa Olimpiki ya Tokyo, Failuna Abdi Mtanga, Gabriel Geay, Angelina Tsere na Ezekiel Ngimba huku Grace Jackson kutoka JKT Arusha akiahidi kuendeleza makali yake kwenye Kilomit 10.     

NBC Dodoma Marathon inatarajiwa kujumuisha Mbio za Kilomita 42, Kilomita 21, Kilomita 10 na Kilomita 5 maarufu kama ‘Fun Run’.

Mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa ‘World Athletics’ zamani IAAF na Chama cha Kimataifa cha Marathon (AIMS), inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), huku ikitarajiwa kushirikisha washiriki 3,000.

Mshindi wa kwanza katika Mbio za Kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake ataondoka na kitita cha Sh. 3,500,000 kila mmoja huku wa pili akijitwalia Sh. 2,500,000 wa tatu 1,500,000 wa nne Sh. 1,000,000 huku wa tano akijitwalia Sh. 750,000 wakati wa sita hadi kumi wakiondoka na Sh. 500,000 kila mmoja.

Kwa upande wa Kilomita 21 mshindi atajipatia Sh. 2,500,000 wa pili 1,500,000 wa tatu 1,000,000 wa nne 750,000 wakati wa tano atajitwalia Sh. 500,000 huku wale wa sita hadi kumi wakiondoka na Sh. 300,000 kila mmoja.

Mbio za Kilomita 10 mshindi atajitwalia kitita cha Sh. 1,000,000 wa pili Sh. 750,000 wa tatu Sh. 500.000 wa nne Sh. 250,000 wakati wa tano atajishindia Sh. 200,000 wakati wa sita hadi kumi wakijipoza na Sh. 100,000.

Kwa upande wa mbio za kujifurahisha za Kilomita 5, washiriki wote watakaofanikiwa kumaliza watajipatia medali.

Ada kujisajili ni Sh. 25,000 ambapo usajili unaendelea katika matawi ya NBC, Shoppers Plaza jijini Dodoma na Mlimani City Dar es Salaam. Kila atakayejisajili pia atapata fulana maalumu ya kukimbilia.

Mbali na kujenga afya na kupromote mchezo wa Riadha, NBC Marathon inalenga kusaidia jamii yenye uhitaji, ambapo kwa mwaka huu mapato yote yatakayopatikana kupitia usajili yatapelekwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusaidia akina mama wanaosumbuliwa na kansa ya shingo ya kizazi.

No comments:

Post a Comment

Pages