Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
Mwavuli Linalosimamia Shughuli za Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari
Mongo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la wadau wa
kilimo hai linalotarajiwa kufanyika Novemba 23/2020 katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM). Kulia ni Mratibu wa Shirika lisilo la
Kiserikali linalojishughulisha na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO),
Abdallah Mkindi. (Picha na Suleiman Msuya)
Mratibu wa Shirika lisilo la
Kiserikali linalojishughulisha na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO),
Abdallah Mkindi akifafanua kuhusu kongamano la kilimo linatarajiwa
kufanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Mwavuli Linalosimamia Shughuli za Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo.
NA SULEIMAN MSUYA
ZAIDI
ya wadau wa kilimo 300 kutoka nchi tano wanatarajiwa kukutana Novemba
23/2020 katika mjadala wa wazi juu ya kuelekea kwenye uhuru wa mbegu na
utunzaji wa bioanuai ya Tanzania.
Kongamano
hilo la siku moja limeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali
linalojishughulisha na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO) na Shirika
Mwavuli Linalosimamia Shughuli za Kilimo Hai Tanzania (TOAM),
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TOAM, Bakari Mongo wakati
akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Mongo
amesema kongamano hilo ambalo linakutanisha wadau 300 kutoka nchi za
Tanzania, Ivory Cost, Bokinafaso, Uswisi na Afrika Kusini limelenga
kuongeza uelewa wa umma kuhusu faida za kutumia mbegu asili kwenye
kilimo.
Amesema kongamano
hilo litafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam hivyo kuwataka wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo
kujitokeza kwa wingi ili kujadili kwa pamoja.
"Zaidi
ya wadau 300 wa kilimo kutoka sekta binafsi, serikali, asasi za kiraia,
washiriki wa maendeleo, wakulima, wanafunzi kutoka vyuo vya elimu ya
juu na waandishi wa habari watakutana na kujadili kuhusu hatima ya mbegu
asili na mkulima wa Tanzania,"amesema.
Amesema
mkakati wa TOAM na TABIO ni kuhakikisha mkulima anayetumia mbegu asili
anathaminiwa na kutambulika na dhana ya kupigia chepuo mbegu
zilizoongezwa vinasaba zisiwepo kwani hazina faida kwa mkulima na mlaji.
Mongo
amesema ni imani yake elimu na mjadala huo vitafungua kurasa mpya kwa
jamii hasa mkulima ambaye wakati mwingine anaingia kwenye mtihani mgumu
wa nini afuate mbegu asili au zenye vinasaba ambazo zinadaiwa kuwa na
athari za kiuchumi.
Mratibu
wa TABIO Tanzania, Abdallah Mkindi amesema, wameamua kuandaa kongamano
hilo kutokana na ukweli kuwa mbegu ni kiunganishi cha kwanza katika
mnyororo wa chakula hivyo ni jukumu lao kizilinda na kuzirithisha kwa
vizazi vijavyo.
"Uzalishaji
wa mbegu na kubadilishana miongoni mwa wakulima imekuwa msingi wa
kutunza bioanuai ya kilimo na uhuru wetu wa chakula," amesema.
Mkindi
amesema mbegu asili ndizo zinaweza kumkomboa mkulima NA wananchi hivyo
ni wakati muafaka kwa nguvu nyingi kuelekezwa huko na kuachana na
mitazamo ya kufikiria mbegu zenye vunasaba.
Amesema
dhana ya kuwa mbegu hizo zinaongeza uzalishaji haina ukweli hivyo jamii
inapaswa kusisitizwa kutumia mbegu asili kwani ndio suluhu ya uhaba wa
chakula duniani.
No comments:
Post a Comment