HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 12, 2020

UPIMAJI SHIRIKISHI WAPAMBA MOTO NYASA

Wananchi wa kijiji cha Likwilu Kata ya Kilosa wakiwa na wataalamu wa Mipangomiji Wilaya ya Nyasa,wakiendelea na upimaji Shirikishi Unaofanyika kati ka kijiji chao.Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeanza Upimaji Shirikishi ili kutatua kero yaw a nanchi wanaoishi katika makazi Holela. (Picha na Ofisi ya DED NYASA).


 Na Netho Sichali

Halmashauri ya wilaya ya Nyasa imeanza zoezi la Urasimishaji wa makazi holela ili wananchi waweze kupimiwa na kumilikishwa kwa kupatiwa hati miliki ya Viwanja vyao. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Bw Jimson Mhagama, wakati akiongea na Mwandishi wa Habari hizi Ofisini kwake leo, wakati akiongelea zoezi la Urasimishaji ambalo linaendelea katika Kijiji cha Likwilu Kata ya Kilosa Wilayani hapa.


Bw Mhagama amefafanua kuwa, Lengo la Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ni Kupanga, kupima, kumilikisha maeneo yote Wilayani hapa ili kuzuia ujenzi holela, kuwezesha kusogeza huduma mbalimbali za jamii na pia kuongeza mapato ya Serikali
kupitia maduhuru mbalimbali yatokanayo na tozo za ardhi. 

Katika upimaji huo viwanja takribani 1500 vinatarajiwa kupimwa. Ameongeza Upimaji huu ni shirikishi kwa mujibu wa Mwongozo wa urasimiashaji wa makazi wa Mwaka 2000 na kwamba Halmashauri ya Nyasa imekuwa Halmashauri ya kwanza Tanzania kushusha gharama za urasimishaji wa makazi hadi kufikia Shilingi 50,000/= kwa kila kiwanja ukilinganisha na gharama elekezi za hapo awali kwamba urasimishaji usizidi kiasi cha shilingi 150,000/= kwa kiwanja kimoja ikiwa ni gharama za
kupanga na kupima.


“Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa tayari imeanza Zoezi la urasimishaji Makazi ya Wananzhi wetu na zoezi limeanza katika kijiji cha Likwilu Kata ya Kilosa na Tunatarajia Zoezi hili lifanyike Halmashauri nzima katika maeneo yaliyo na sifa za kufanyiwa urasimishaji wa makazi”
 

Amezitaja faida za Urasimishaji kuwa ni Kuondoa Migogoro ya Ardhi, kupata hati Miliki ambazo zitawasaidia kuweka rehani katika Taasisi za Kifedha, kupangwa kwa eneo kimipango miji, Kufikiwa na Huduma muhimu kwa Urahisi kama Umeme,maji na barabara.
 

Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kushirikiana na wataalamu wa mipango miji wilayani hapa, kuhakikisha wanapima maeneo yao ili waweze kupata maendeleo na kuishi katika eneo ambalo limepimwa na lenye Miundombinu ya kutosha.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Likwilu wakiongelea upimaji huo wamesema wanaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, kwa Kuanza zoezi la Urasimishaji wa makazi yao kwa kuwa awali walikuwa wanaishi kwenye makazi holela ambayo ilikuwa haina miundombinu kama barabara, maji, umeme hali iliyokuwa inawalazimu hata kuuza kwa bei rahisi na kukosa dhamana wanapokuwa na uhitaji wa kukopa Benki.


Mara baada ya Upimaji wanategemea kuuza kwa bei ya juu Viwanja vyao na maeneo yatapanda thamani kubwa,” Kwa kweli tunaipongeza sana Halmashauri ya Nyasa kwa Kurasimisha makazi yetu ,tumepatiwa elimu ya kutosha katika mikutano ya Hadhara na wananchi wamepokea elimu hii vizuri na wamefarijika sana hasa kwa fedha ambayo tutachangia ambayo ni sh 50,000 ambayo wananchi wote wanaouwezo wa kuchangia “alisema Bwana Omary Mkachaga ambaye ni mkazi wa kijiji cha Likwilu.


Ameiomba Serikali kuhakikisha mpango huu unawafikia wananchi wote wa Wilaya ya Nyasa kwa kuwa unalengo la kutatua changamoto iliyowakumba wananchi hao kwa
muda mrefu kwa kuwa walikuwa hawajui kama kiwango cha kupima kimepungua mpaka kufikia elfu hamsini kwa Kiwanja kimoja. Kwa kuwa awali walishindwa kutokana na bei kubwa ya kupimia kiwanja kimoja kuwa juu.


Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini wananchi wengi wameufurahia mpango huu na washirikiana na wataalamu kikamilifu na kuhamasishana wao kwa wao ili kutekeleza mpango huu wa urasimishaji.

No comments:

Post a Comment

Pages