Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti kuhusu dhana ya jinsia ilivyotekelezwa kwenye miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamiii (USMJ), Profesa John Jeckoniah akifafanua utafiti huo mbele ya wadau wa misitu nchini.
Wadau wakifuatilia kwa kina ripoti ya utafiti kuhusu dhana ya jinsia kwenye Miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inayoteklezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG).
Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa akichangia mada baada ya kupokea ripoti ya utafiti kuhusu dhana ya jinsia kwenye Miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu Tanzania (USMJ).
Profesa Suzana Augustino akifafanua jambo juu ya utafiti wao waliofanya kuhusu Miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu Tanzania (USMJ) inayoratibiwa na TTCS kupitia TFCG.
NA SULEIMAN MSUYA
UTAFITI umeonesha dhana ya uwezeshaji wanawake kijinsia inayotekelezwa kwenye miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) ni changamoto kwa baadhi ya wanaume wa vijiji husika.
Akizungumza baada ya kuwasilisha matokeo ya utafiti waliofanya katika vijiji 10 na wilaya tatu za Kilosa, Morogoro na Mvomero mkoani Morogoro, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Profesa John Jeckoniah amesema wanaume wengi wana hofu na uwezeshaji wanawake kupia miradi ya USMJ.
"Vijiji ambavyo tumefanikiwa kufika ni Ulaya Mbuyuni, Ihombwe, Ng'ole, Muhenda na Chabima vya Kilosa, Mlilingwa na Kiwege Morogoro na Ndole, Masimba na Maharaka Mvomero," amesema.
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) unaoratibiwa na Shika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Prof.Jeckoniah amesema utafiti huo ambao alishirikiana na Profesa Suzana Augustino umebaini mambo mengi ambayo ni ya chanya kwa jamii ila changamoto zipo ikiwemo hiyo ya wanaume kuhofia uwezeshaji wanawake.
Amesema kwa mujibu wa utafiti huo baadhi ya wanaume wa vijiji 10 ambavyo wamefika wanaona mradi wa TTCS umeharibu mila na tamaduni zao kuhusu nafasi ya mwanamke pamoja na mafanikio wanayoyaona hivyo nguvu iongezwe katika kuwajengea dhana ya jinsia na umuhimu wake.
"Tulipowauliza wanaume ni kwa namna gani wamepokea miradi ya USMJ wanasema ni mizuri lakini baadhi ya wanawake ambao wanashiriki katika mpango hisa wameanza kutowasikiliza jambo ambalo wanaamini limechochewa na mradi ila kiuhalisia ni uelewa mdogo," amesema Prof.Jeckoniah.
Mhadhiri huyo amesema kinachohitajika ni elimu zaidi kutolewa kwa pande zote ili dhana hizo ziondoke na kujikita kwenye dhana ya jinsia kama njia ya kuchochea maendeleo.
Amesema dhana ya 50/50 inapaswa kueleweka kwani miradi hiyo ya USMJ inaonekana kuwapa ujasiri baadhi ya wanawake kutamani kuomba talaka jambo ambalo sio matarajio ya miradi.
Aidha, Prof. Jeckoniah amesema utafiti huo umeonesha mafanikio makubwa sana kwenye jamii husika hivyo kuwataka wadau kuendelea kusisitiza usawa wa kijinsia katika maeneo yote nchini hasa kwenye miradi ya uzalishaji.
Kwa upande wake Prof.Augustino amesema utafiti umeonesha wanawake ambao hawajaolewa au kuachika wamekuwa washiriki wazuri kwenye USMJ jambo ambalo linathibitisha changamoto iliyopo kwa wanaume pamoja na kuona manufaa.
Amesema kwa ujumla wanaume wanaonekana kuwa wanufaika wakubwa kwa kuwa wao ndio washiriki ila dhana ya jinsia inatekelezwa kwa kiwango kizuri.
Amesema pia idadi ya wanawake katika baraza ya vijiji na kamati mbalimbali imekuwa ikiongeza hivyo dhana ya jinsia inazidi kukua siku hadi siku.
Halikadhalika amesema kuna changamoto kwa wanawake kumiliki ardhi pamoja na uwezekano wa kuipata kuwepo.
"Utafiti unaonesha mume na mke wana uwezo wa kuwa na ardhi ila tatizo ni kwa mwanamke kuwa na maamuzi nayo hivyo bado kuna changamoto ya jinsia hapa," amesema.
Prof.Augustino amesema changamoto nyingine ambayo wanawake wanakutana nayo ni wanawake kushindwa kuandaa tanuri mpaka wawalipe wanaume jambo ambalo linapunguza faida.
Amesisitiza kuwa kufikia 50/50 katika masuala ya kijinsia inahitaji muda wa kutoa elimu zaidi kwa pande zote kuanzia ngazi ya chini.
Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa amesema pamoja na changamoto ambazo zimeoneshwa na watafiti hao ni wazi miradi ya USMJ imeonesha dhana ya usawa na uwiano kuanza kutokea kwa wanavijiji wanaozungukwa na misitu.
"Haya ambayo yameoneka kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiungozi na kijinsia kupitia utafiti ni dhahiri USMJ inamchango mkubwa hivyo iwapo utafiti huu na nyingine zinafanyiwa kazi kuna mabadiliko yataoneka," amesema.
Naye Mtafiti Dk.Aman Uisso wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), amesema utafiti huo umegusa masuala muhimu ambayo yatabadilisha jamii kupitia rasilimali zao kwa usawa na uwiano.
Amesema jambo la msingi ni kuhakikisha mambo yote ambayo ni muhimu yanatekelezwa na kila mdau anayehusika.
Ofisa Misitu Wilaya ya Kilolo, Robert Sigge amesema utafiti huo pamoja na mazuri yake unapaswa kufikiwa wadau wote hasa wafanya maamuzi kwani hakuna shaka dhana ya jinsia ni chachu ya maendeleo.
Edward Kimweri Ofisa Misitu wa Wilaya ya Mvomero amesema matokeo ya utafiti huo pamoja na kuainisha dhana ya jinsia pia umeonesha rasilimali zinazozunguka jamii zitakuwa endelevu kwa mfumo huo wa kuwepo kwa usawa na uwiano.
"Miradi ya USMJ ambayo imetekelezwa na TTCS inaonekana kuwa endelevu kutokana na dhana ya jinsia ambayo imetolewa hivyo wenye hofu wataendelea kuelewa kidogo kidogo.
Ofisa Maliasili Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo amesema matokeo ya utafiti huo yanatoa matumaini na nguvu kwa watendaji wanaosimamia rasilimali misitu kutetea hoja ya USMJ.
Mtimbanjayo amesema manufaa ya utafiti huo yatazingatia mapokeo ya wafanya maamuzi na kuwaomba TFCG kuangalia uwezekano wa kuandika taarifa hizo kwa lugha inayoeleweka.
Meneja Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST), Charles Leonard amesema awamu ya kwanza na pili ya mradi wa TTCS ilizingatia dhana ya usawa na uwiano wakiamini ndio njia ya kuchochea mabadiliko.
"Sisi tangu awali tulikuwa tunaamini dhana ya jinsia ndio njia ya kufanikisha mradi ufanikiwe hivyo tutahakikisha kwenye mradi wa CoFoREST unajikita huko zaidi," amesema.
Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo amesema wamekuwa wakitoa kipaumbele kwenye utafiti wakiamini ni njia sahihi ya kuwaonesha mafanikio na mapungufu kwenye miradi yao.
Amesema wanatumia watafiti kutoka SUA kwa kuwa hilo ni eneo lao walilobebea wakiamini watakuja na majibu halisi ya mafanikio na mapungufu.
"Tunafanya utafiti tukiamini wafanya maamuzi na watunga sera watachukua na kuufanyia kazi kwa maslahi ya wananchi na nchi kwa ujumla, lakini pia tunatekeleza ule msemo wa bila utafiti huna haki ya kupinga au kuzungumza," amesema.
Amesema TFCG kupitia mradi wa TTCS na CoFoREST wanahusisha wilaya saba ambazo ni Kilosa, Morogoro, Mvomero, Kilolo, Ruangwa na nyingine.
No comments:
Post a Comment