Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akitoa hotuba ya ufunguzi mbele ya Makatibu Wasaidizi wa TSC (hawapo pichani) kutoka Wilaya mbalimbali za Tanzania Bara wakati wa Kikao cha Kazi cha Makatibu Wasaidizi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma.
Na Mhina Adili, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba amewataka watumishi wa Tume hiyo kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili kuwezesha walimu anapatiwa huduma kwa wakati.
Prof. Komba alitoa kauli hiyo katika kikao kazi kilichowahusisha Makatibu Wasaidizi kutoka Wilaya zote za Tanzania bara kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Chuo cha Mipando jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi katika kutekeleza majukumu yao.
Alieleza kuwa wapo baadhi ya watumishi wa Tume ambao wamekuwa ni kikwazo katika ustawi wa walimu huku akisisitiza kuwa Tume ilianzishwa kwa lengo la kumsaidia mwalimu ili aweze kuwa na ustwawi mzuri katika utumishi wake.
Aliweka bayana kuwa kumekuwa na vitendo mbalimbali vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma kwa baadhi ya watendaji wa TSC huku akisisitiza kuwa katika kipindi cha uongozi wake hatomvumilia mtumishi yeyote asiyetaka kufanya kazi kwa mujibu wa Taratibu.
“Wapo baadhi yenu ambao tumepata taarifa zao na tumeanza kuwachukulia hatua kutokana na kutozingatia maadili ya kazi. Unakuta Katibu Msaidizi anaomba rushwa kwa mwalimu mwenye mashauri ya nidhamu ili hata kama ana hatia wasimpe adhabu”, alisema prof. Komba.
Aliongeza kuwa hata katika mchakato wa kuwapandisha madaraja walimu wapo baadhi ya watumishi wanaojihusisha na rushwa kwa lengo la kutoa upendeleo kitu ambacho sio kwamba tu ni kinyume na sheria lakini kinadhalilisha Utumishi wa Umma.
Katika kushughulikia mashauri ya nidhamu, prof. Komba alieleza kuwa katika kipindi ambacho amekaa Tume kama mwenyekiti amebaini kuwa zipo changamoto kwa Makatibu Wasaidizi na Kamati za Wilaya katika kuendesha mashauri ya nidhamu kwa walimu.
“Nimeona rufaa zinakatwa na walimu kupinga maamuzi yanayofanywa na Kamati za Wilaya. Rufaa nyingi zinakubaliwa na uamuzi wa kamati za wilaya unatenguliwa lakini ukiangalia sababu kubwa za rufaa kukubaliwa ni kutozingatiwa kwa Kanuni na Taratibu wakati wa kuendesha mashauri”. Alisema Mwnyekiti huyo.
Alisema Tume imeamua kuendelea kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi katika kufahamu Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na Kanuni zake ili kuongeza weledi katika uendeshaji wa mashauri ya nidhamu wilayani.
No comments:
Post a Comment