NA MWANDISHI WETU, TANGA
SERIKALI imeendelea kuziwezesha taasisi mbalimbali za utafiti zikiwemo za mifugo ili kusaidia kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwainua kiuchumi.
Baadhi ya vituo vya utafiti vilivyowezeshwa na serikali kwa kupatiwa ruzuku kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ni Kituo cha Utafiti wa Mifugo Tanga kilicho chini ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) ambacho kilianzishwa miaka ya 1950.
Kituo hicho kilikuwa na jukumu la kufanya utafiti wa malisho ya mifugo katika Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Akizungumzia kuhusu hilo, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho Elibariki Masakia amesema,Taasisi hiyo ni kongwe na imekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo pamoja na miundombinu ya kufanya utafiti hivyo kupelekea kuwepo kwa uhitaji wa ukarabati na ujenzi wa majengo mapya ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema kutokana na mahitaji hayo kituo kiliomba ruzuku kutoka serikalini kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kufanya maboresho ya maabara, jengo la kufundishia kwa vitendo ufugaji kuku wa kisasa, chumba cha kupozea pamoja na mizani ya kisasa ya kidijitali ya kupimia wanyama.
Amesema serikali imefanya kazi kubwa katika mahitaji hayo ambapo baadhi ya majengo yameshajengwa na sasa ufungaji wa mizani ya kidijitali upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ambapo mfumo huo utakapokamilika utawezesha kutambua uzito wa mfugo ambao ni muhimu kwa kila mfugaji, daktari wa mifugo na hata watafiti.
“Kipimo hiki husaidia kutambua maendeleo ya afya ya mfugo husika, kuandaa chakula kinachoendana nayo, kukadilia dozi ya dawa pindi mfugo ukiugua na kukadilia kiwango cha mazoezi anayohitaji kwa ajili ya uzalishaji wenye tija”amesema Masakia
Masakia amefafanua kuwa ruzuku iliyotolewa na serikali kupitia COSTECH imesaidia taasisi hiyo katika utekelezaji wa miradi hiyo na kukiwezesha kituo kudhibiti ubora wa mazao ya mifugo na malisho kwa mikoa ya Kanda ya Pwani.
Hata hivyo mradi huo unaojumuisha miundombinu mitatu ni muhimu kwa kuwa unaleta tija kwa wadau wa sekta ya mifugo kuanzia taasisi yenyewe, wafanyakazi wake, wakulima, wazalishaji na waagizaji wa chanjo.
No comments:
Post a Comment