HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 11, 2021

NHIF SINGIDA MBIONI KUNUFAISHA WAKULIMA 300 KUPITIA ‘USHIRIKA AFYA



Meneja wa NHIF  Mkoa wa Singida,, Dk. Mohamedi Kilolile.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia fao lake mahsusi kwa wakulima wa Pamba linalojulikana kama ‘Ushirika Afya’ unatarajia kuanza kutoa huduma ya matibabu kwa wakulima takribani 300 wa zao hilo kwa gharama ya shilingi mia mbili (200) kwa siku ambazo ni sawa na 76,800 kwa mwaka.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa (NHIF) mkoani hapa, Dk. Mohamedi Kilolile, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, hivi karibuni.

“Niwaombe wakulima wa pamba wachangamkie fursa hii kwa kujiandikisha ili kupata huduma ya fao hili la ‘ushirika afya’ sababu maradhi hayapigi hodi. Sifa za kupata huduma hii ni sharti kwanza uwe mkulima wa pamba na pili uwe mwanachama wa amcos,” alisema Kilolile. 

Alisema gharama ya fao hilo kwa mkulima mmoja ni shilingi 76,800 kwa mwaka huduma ambayo imetajwa kuwa na gharama nafuu zaidi ambayo kwa mgawanyo wa malipo ya gharama husika kwa mwaka ni sawa na mkulima kulipia shilingi 200 tu kwa siku.

Kilolile alieleza kuwa kwa sasa huduma hiyo imekwishaanza kutolewa kwa maeneo mengine, ambapo NHIF kwa kushirikiana na Benki ya Posta nchini (TPB) vimeungana ili kurahisisha utoaji wa fao hilo kwa utaratibu wa benki husika kumuazima huduma husika mkulima na kisha kurejesha malipo ya huduma hiyo baada ya kuuza mazao yake.

“Mpaka sasa mkoa wa Singida tumekwisha tembelea Amcos 31 na kufanikiwa kuandikisha wanachama wake 300 wanaojishughulisha na kilimo cha zao la pamba na zoezi bado linaendelea kabla ya mfuko kwa kushirikiana na TPB kuanza kuwanufaisha na fao hili,” alisema.

Aidha, akizungumzia huduma nyingine zinazoendelea kutolewa mpaka sasa kwa watanzania wote na zilizofanyiwa maboresho, Kilolile alisema mpaka sasa mfuko huo unatoa huduma ya vifurushi vya aina 3 vinavyoendana na ngazi ya uchumi wa kila mteja kuweza kumudu gharama yake kwa ubora stahiki.

Alivitaja vifurushi hivyo kuwa ni kile cha ‘Najali’ ambacho gharama yake kwa mtu mmoja ni shilingi 192,000 kwa mwaka, pia kifurushi kingine ni ‘Wekeza’ ambacho gharama yake kwa mtu mmoja ni shilingi 384,000 kwa mwaka na ‘Timiza’ ambacho huduma yake kwa mwaka kwa mtu mmoja  ni shilingi 516,000.

Pia alisema huduma ya vifurushi vyote hivyo hutolewa kwa mgawanyo wa makundi rika kwa kati ya umri wa miaka 18-35, 36-59 na zaidi ya 60. Aidha, fursa nyingine ya vifurushi hivyo mathalani ‘Najali’ pamoja na kugharamia huduma ya Bima ya Afya kwa mwaka mzima pia hutoa fursa ya mgonjwa kupatiwa huduma ya kulazwa wodini kwa siku 30, huku ‘Wekeza’ ikitoa siku 45 na ‘Timiza’ kikitoa siku 60 kwa huduma hiyo ndani ya mwaka. 

“Chaguo ni lako. Niwasihi wana-singida na watanzania kwa jumla changamkieni huduma hizi kwa ustawi wa afya katika muktadha wa ujenzi imara wa taifa letu. Ugonjwa huwa haumuandai mtu…unaweza kuazima nauli ya kwenda mahali fulani na ukapewa lakini huwezi kuazima fedha ya kwenda kwenye matibabu kwa sababu hujui matibabu hayo yatagharimu kiasi gani cha fedha,” alisema Kilolile. 

No comments:

Post a Comment

Pages