NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA
SERIKALI ipo kwenye hatua za mwisho za kuhakikisha kunakuwepo na uondoshaji mkubwa wa maji taka katika jiji la Dodoma unaojumuisha ujenzi wa kilomita 250 za mabomba pamoja na mabwawa 16 yatakayojengwa katika eneo la Nzuguni.
Hayo yamesemwa leo Jijini hapa na Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi alipokuwa akifungua Baraza la Sita la wafanyakazi wa DUWASA ambapo amesema lengo ni kuifanya Dodoma kuwa na sura ya Makao Makuu ya nchi.
Amesema ili mradi huo ufanikiwe kwa malengo yaliyokusudiwa lazima wananchi wapatiwe elimu ya kutosha kwani ni wachache wanaofahamu kuwa wanaweza kuunganishiwa mfumo huo kutoka kwenye makazi yao hadi kupeleka maji taka kwenye mabwawa.
"Duwasa inatakiwa kutatua kero kwani kero nyingine zimekuwa zikisababishwa na baadhi ya watu ambao wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi,".
Na kuongeza kusema" Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika kutokana na huduma wanazozipata hivyo kupitia baraza hili hakikisheni mnafanya kazi ya kuzitatua kero hizo ili wananchi wafurahie uwepo wa mtandao wa maji," amesema Waziri Maryprisca.
Amesema kuna kila sababu ya Duwasa kuendelea kuujenga mtandao wa maji kwa kuwafikishia wananchi huduma za maji kwani wanauhitaji huo .
"Wizara itaendelea kuiwezesha ili iweze kutoa huduma bora kwa Wananchi," Amesema Waziri huyo.
No comments:
Post a Comment