Vijana wa Chama cha Skauti Mkoa wa Mbeya wakikarabati kivuko cha watembea kwa miguu katika Mtaa wa Mayombo Kata ya Iwambi baada ya kuharibiwa na mafuriko.
Vijana wa Chama cha Skauti Mkoa wa Mbeya wakiwajibika.
Na Dotto Mwaibale
KUTOKANA na mvua zinazo endelea kunyesha Mkoa wa Mbeya na kuharibu miundombinu ya barabara Chama cha Skauti mkoani humo kimeendelea kutoa huduma ya kukarabati miundombinu hiyo kwa wathirika wa mafuriko.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole alisema mvua iliyonyesha Januari 23 mwaka huu ilileta athari kubwa kSatika Kata ya Iwambi na kuharibu miundombinu mbalimbali.
Alisema kufuata hali hiyo walikaa na kuratibu namna ya kufika katika maeneo hayo kutoa msaada ambapo kikosi cha uokoaji cha skauti wapatao 16 walikwenda kutoa huduma ya kusafisha mitaro na makaravati.
" Mafuriko hayo yalisababisha athari za kubomoa kuta za nyumba za wakazi wa tatu wa eneo hilo na kuharibu vivuko vya watembea kwa miguu na kuleta changamoto ya matumizi ya barabara kwa wakazi na wanafunzi waishio mtaa wa Mayombo na mitaa jirani ambao wanasoma katika Shule ya Sekondari Sinai, Nsenga, Maziwa, Stella Farm na Shule ya mmMsingi ya Iwambi." alisema Ntole.
Mratibu wa Majanga, Uokoaji na Hali hatarishi wa chama hicho mkoani humo, Lusajo Sanga alisema kazi hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano kutoka kwa viongozi wao.
Alisema kazi kubwa walioifanya ilikuwa ni kurekebisha miundombinu ya kupitisha maji ambayo ilijaa taka na kusababisha maji kutoka nje ya mkondo wake na kuingia kwenye makazi ya watu na kujenga vivuko vya waenda kwa miguu.
Alisema kazi hiyo walifanya kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mayombo akiwepo Mwenyekiti Philipo Mbembati, Mjumbe wa mtaa huo, James Ngungula pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Sanga aliwataja skauti walioshiriki kazi hiyo kuwa ni Kamishna wa Skauti Mkoa Mbeya, Sadock Ntole, Mratibu wa Habari na Mawasiliano Mkoa Mbeya Barnaba Moses, Waratibu wa Skauti Wilaya ya Mbeya, Baraka Martin, Emanuel Mwasikili na Stephano Mwangosi.
Aidha Sanga aliwataja kwa majina skauti waliounda kikosi kilichoshiriki kufanya kazi hiyo kuwa ni Evaristo Sanga, Glory Augustino, Beckam Frank, Elika Mwakabana, Skauta Macklin Lamsi, Elisha, Ckelvi Ekela, Bambo Ekela na Ali.
Sanga alitumia fursa hiyo kusema kwamba Skauti mkoani humo wapo tayari kutoa huduma kwa jamii pamoja na elimu ya jinsi ya kuepukana na athari zitakazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole alitoa rai kwa wananchi na wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya kuchukua tahadhari na kuhakikisha miundombinu ya mitaro na makaravati inayopitisha maji inakuwa Safi na salama wakati wote ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi katika mkondo wake ambapo pia aliwasisitiza wanaozalisha taka wazipeleke kwenye maghuba sahihi ya kuhifadhia ili kurahisisha ubebaji wa taka hizo na kuzipeleka kwenye dampo kuu.
No comments:
Post a Comment