Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinawaomba wadau husika kufuata mazuri ya mwaka jana kuhusiana na kesi za udhalilishaji na kuacha mabaya wakati wa kushughulikia kesi za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Mambo
yaliyokwenda vizuri mwaka jana ni pamoja na kesi ya shambulio la aibu
kutolewa hukumu kwa muda mfupi na yaliyokwenda vibaya ni watuhumiwa
kuachiwa huru, wengine kupewa adhabu ndogo na kesi kuchukuwa muda mrefu
bila kutolewa hukumu.
Kesi ya mtoto wa miaka tisa
(9 ) aliyedaiwa kufanyiwa shambulio la aibu na Juma Haji Ali (25)
mkaazi wa shehia ya Mahonda Mwembe Mazizi ambayo imechukua muda wa wiki
moja tu kukamilika kutoka kuripotiwa hadi kutolewa hukumu, Septemba
22, 2020 hadi Septemba 28,2020.
Juma amepewa adhabu
ya kutumikia kifungo cha miaka saba pamoja na kulipa faini ya shillingi
milioni moja kama ilvyoendeshwa na Hakimu Faraji Shomar Juma wa ya
mahakama ya mkoa Mahonda.
Ilidaiwa kuwa Juma
alimshambulia mtoto huyo wa kike kwa kumuingiza ndani chumba bovu na
kumfanyia kitendo cha kumdhalilisha kwa bahati nzuri mtoto huyo alipiga
kilele hivyo watu wakiwemo wanaharakati walisikia na kuanza kuifuatilia.
TAMWA
ZNZ kwa kuliona hilo inaamini kwamba vyombo vya sheria vina uwezo
mkubwa katika kukabiliana na matukio hayo bila ya kuchukua muda mrefu na
tunavipongeza vyombo vya sheria kwa hilo, ambapo kesi baadhi ya wakati
huchukua zaidi ya miaka miwili. Tunaviomba vyombo vya sheria kutumia
kesi hii kama ni muda halisi wa kuendesha kesi kama hizo katika mwaka
huu wa 2021 na kuendelea.
Hii itasaidia kutisha
wabakaji kwamba hatua zinachukuliwa, itaongeza pia upatikanaji wa haki
pamoja na kuwapa moyo mashahidi kuwa hawatatumia muda mrefu katika
kufuatilia kesi zao.
Kwa
upande wa mambo yaliyokuwa vibaya ni pamoja na kujitokeza kwa uhalifu
mpya ambao ni kuwachoma watoto sindano ambapo kadhia hiyo iliwakumba
watoto tisa (9) sihaba wazazi wa watoto walifanikisha kumpata mtuhumiwa
huyo.
Mhalifu mmoja aliyejulikana kwa jina la Salim Ali Malik ambaye
ilithibitika Mahakamani kuwa aliwachoma watoto sita huko Daraja bovu na
tarehe 24/8/2020 aliweza kubakia huru baada ya Mahakama ya Mwanzo ya
Mwanakwerekwe kumuamuru mtuhumiwa kulipa shilingi laki 600,000 au kwenda
kutumia kifungo cha miezi sita ambapo alilipa fidia hiyo.
Hivyo
adhabu hiyo hailingani na kosa, kwani kitendo cha kuwachoma watoto
sindano bila ya sababu ni uhalifu mkubwa wa kuwaumiza watoto kimwili na
kisaikolojia.
Kwa mujibu wa wazazi ambao walihangaika kujua nini hasa
dhamira ya kuchomwa sindano huko ni kwamba sindano hiyo inaweza kuwa ina
sumu lakini hata hivyo walisema hukumu ilitolewa bila ya ripoti ya
Mkemia Mkuu kusomwa Mahakamani.Watoto wengine watatu waliobakia
walifanyiwa kitendo hicho huko shehiya ya Mwanyanya, Unguja.
Halikadhalika,
Disemba mwaka jana (2020) Mahakama ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba
ilimwachia huru bila ya sharti lolote mtuhumiwa Salim Khamis Ali maarufu
‘Panga la shaba’ (43) mkaazi wa Taifu shehia ya Kinyasini aliyedaiwa
kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa chini ya miaka 13 huko Pemba
kutokana na kukinzana kwa muda ambapo shahidi alisema alibakwa muda wa
saa 10 jioni na hati ya mashtaka ilisema ni saa 3 za usiku na kwamba pia
mtoto alikuwa ana sitasita.
Vile vile kesi za
mauwaji ya wanawake zinaendelea kuchukua muda mrefu tangu ziliporipotiwa
hali ambayo inakatisha tamaa kwa familia pamoja na jamii nzima ya
wanawake kutokana na kuishi kwa khofu na pia uwezekano wa wahalifu
kukimbia hukumu.
Kwa mujibu wa rikodi za TAMWA ZNZ
tangu mwaka 2016, matukio 17 ya mauwaji ya wanawake yameripotiwa ambapo
ni matukio tatu (3) tu ndiyo yaliyofikishwa katika Mahakama Kuu ya
Zanzibar, ambapo kesi ya Wasila Mussa (21) na Hajra Abdallah Abdallah
(21) zipo mahakamani, kwa upande wa kesi ya Samira sultan (56)
imeondolewa na mahakama kwa kile kilichoelezwa ni kutokana na mashahidi
kutofika mahakamani kutoa ushahidi.
Tunaamini kuwa
mwaka 2021 taasisi na wadau husika zitajipanga vizuri kwanza kulinda
wanawake na watoto ili wasifanyiwe vitendo hivi viovu na pia kuhakikisha
kuwa hukumu kali zinachukuliwa na kwa muda muafaka dhidi ya wakosaji
wote.
No comments:
Post a Comment