HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2021

WALIMU WAKUU LUDEWA WAUKUBALI MRADI WA DARASA JIFUNZE

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Shaurimoyo, Senebius Mtega akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Maholong'wa, Bw. Chefasi Mdessa akizungumza ofisini kwake hivi karibuni.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Matika, Ludan Njuu (kushoto), kulia ni mmoja wa walimu maalum wa kujitolea wa darasa la jifunze shuleni hapo.  

Na Joachim Mushi, Ludewa

 

BAADHI ya walimu wakuu wa shule za msingi zinazotekeleza mradi wa majaribio wa Darasa Jifunze ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe wameomba mradi huo uwe endelevu ili kuwasaidia wanafunzi wanaokubwa na changamoto ya ujifunzani hadi kufika darasa la tatu na kuendelea wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni wilayani Ludewa kwa nyakati tofauti na walimu hao katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia maendeleo ya mradi wa darasa jifunze uliokuwa ukitekelezwa kwenye shule zao.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Maholong'wa, Bw. Chefasi Mdessa akizungumza amesema kuna mafanikio makubwa ya mradi huo unaotekelezwa kwa majaribio katika shule hiyo, jambo ambalo limeleta matumaini kwao na hivyo kushauri ikiwezekana mradi huo uendelee kutekelezwa katika shule za msingi zenye changamoto ya ujifunzaji. 

Alisema tathimini iliyofanywa kubaini wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kuanzia darasa la kwanza hadi la sita katika shule hiyo, ilibainini wanafunzi 83 wakiwa hawajui kusoma vizuri na hivyo kuingizwa rasmi katika mradi wa Jifunze uliotekelezwa kwa awamu tatu zenye siku 10. Alisema ndani ya siku 30 za utekelezaji mradi huo ilifanikisha kuwawezesha idadi kubwa ya wanafunzi na kusalia 9 tu ambao walikuwa bado na changamoto hiyo.

"...Mapendekezo mengine binafsi natamani mradi huu uwe wa kudumu shuleni hapa na utumike kwa kufundishia darasa la awali, darasa la kwanza na kwa darasa la pili, naamini mafanikio tulioyapata kwa muda mfupi tukiingiza mfumo huu ukawa wa kudumu tutapunguza kwa kiasi kikubwa wanafunzi waliojua kusoma na kuandika katika shule zetu," alisema Bw. Chefasi Mdessa.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Shaurimoyo, Senebius Mtega alisema mradi wa darasa la Jifunze ulianza kutekelezwa katika shule hiyo tangu mwezi Agosti 2020 ukiwa na wanafunzi 78 wasiojua kusoma na kuandika katika hatua mbalimbali ulikuwa na mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi. Alisema wapo wanafunzi ambao walikuwa wanashindwa kusoma herufi, wengine pia kushindwa kusoma maneno na pia wapo ambao walishindwa kusoma aya; ambapo waligawanywa kulingana na changamoto zao za ujifunzaji lakini idadi kubwa ilifanikiwa.

"...Tulianza kutekeleza mradi tukiwa na wanafunzi 78, kimsingi mradi huu umetusaidia sana kwani wanafunzi wengi wamefaulu kutoka katika changamoto ya awali ya kutokumudu kusoma na kuandika kwa ufasaha. Ni mradi mzuri tunaupenda na tunapenda hata uwe endelevu hapa kwetu na hata kwenye shule zingine," aliongeza Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Shaurimoyo, Bw. Mtega.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Matika, Ludan Njuu anasema hadi wanaanza kutekeleza mradi wa Jifunze walikuwa na jumla ya wanafunzi 75, waliokuwa na changamoto za usomaji kwenye madaraja ya aya, maneno na silabi, lakini hadi mwisho wa mradi zinakamilika siku 30 ni wanafunzi 13 pekee ndio walikuwa na changamoto hiyo, huku wengine wote wakifanikiwa kuvuka katika changamoto hiyo.

"...Kimsingi zoezi hili kama litaendelea watoto wengi walio na changamoto hiyo tunaweza kuwapunguza. Alishauri viongozi sekta ya elimu kwa kushirikiana na Uwezo Tanzania kuangalia namna ya kuufanya mradi huo uwe endelevu na kutekelezwa shule zote kwa madarasa ya awali, darasa la kwanza na la pili ili kumaliza kabisha changamoto hiyo ambayo ipo katika maeneo kadhaa," alisema mwalimu huyo.

No comments:

Post a Comment

Pages