HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 09, 2021

Waziri Wang: China Inakaribisha Samaki kutoka Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia utiaji Saini wa mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga km 341 kati ya Shirika la Reli Tanzania TRC kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Masanja Kadogosa na
Ubia wa Kampuni mbili za Kichina, China Civil Engineering Construction Corporation CCECC na China Railway Construction Corporation Limited CRCC kupitia Mtendaji Mkuu wa CCECC Zhang Junle katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita leo tarehe 08 Januari 2021.

 

 

Na Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato

 
Waziri wa Mambo ya Nje wa China,Wang Yi amesema kuwa
nchi yake inakaribisha samaki kutoka Tanzania kuuzwa moja
kwa moja nchini humo ili kusaidia sekta ya maendeleo ya
uvuvi nchini.


Akizungumza jana (Januari 8, 2021) wakati alipotembelea
Mwalo wa Chato beach uliopo katika Wilaya ya Chato mkoani
Geita, na kukutana na wavuvi Waziri huyo wa Mambo ya Nje
wa China alisema kuwa soko la samaki China ni kubwa na
hivyo anakaribisha samaki kutoka Tanzania kuuzwa nchini
kwake.


“Nimeambiwa wakati wa mvua Tanzania hali inakuwa ngumu
sana na soko la samaki huko China ni kubwa. Kwa hiyo
ningependa kutangaza kwamba China inakaribisha samaki
kutoka Tanzania na pia tungependa kuwasaidia kuongeza
mapato na kuboresha maisha yenu”.


Alisisitiza “Tunapenda kusaidia kuuza bei ya samaki watanzania
kupitia mkataba husika ili mazao kutoka Ziwa Victoria yaende
China kwa urahisi zaidi.”
Vilevile, Waziri Wang alisema kuwa Ubalozi wa China nchini
utatoa kiasi cha dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kusaidia
wavuvi wa mwalo wa Chato kununua vifaa vya uvuvi.
Aidha, alionesha kufurahishwa na zawadi ya samaki aliyopewa
na wavuvui wa mwalo huo .

“ Leo nyinyi mmenizawadia samaki wazuri na wakubwa sana,
nimefurahi sana na nashukuru sana, kitendo hili kinaonesha
hisia zenu na urafiki wa kweli.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashamba
Ndaki alisema kuwa Tanzania imejaliwa rasilimali za uvuvi
katika maeneo mbalimbali ya maziwa, mito na bahari ambazo
zinachangia pato la taifa, ambapo asilimia 75 ya mazoa ya
uvuvi yanayozalishwa hapa nchini yanavunwa kutoka Ziwa
Victoria.


Waziri Ndaki alitaja mazao hayo matatu ya kibiashara kuwa ni
samaki aina ya sangara, sato na dagaa. “Mazao yatokanayo na samaki aina sangara yanayojumuisha minofu na mabondo ndio husafirishwa kwa wingi kwenda kwenye soko la kimataifa ikiwemo China, kwa kupitia Hong Kong. 

Ni lengo la serikali yetu kuuza zao hili moja kwa moja
nchini China.”alisema Waziri Ndaki Alifafanua kuwa matarajia ya Serikali ni kusaini mkataba utakaowezesha kuuza bidhaa hizo moja kwa moja katika soko la China.


“Tunaomba mheshimiwa Waziri Wang mara tutakapowasilisha
rasmi maombi ya soko la mabondo tuungwe mkono na Serikali
ya China. Tuna imani kwamba kufunguliwa kwa soko hilo
kutasaidia sana jitihada za wananchi kujikwamua na umasikini”
alisisitiza Waziri Ndaki.


Tanzania ina mialo 1,373 ikiwamo mwalo wa Chato licha ya
Serikali kufanya juhudi za kuendelea mialo hiyo hapa nchini
bado kuna fursa ya kuboresha miundombinu ya kupokea,
kuhifadhi na kuchakata mazao ya samaki.

Aidha, Waziri Ndaki aliiomba Serikali ya China kuhamasisha
makampuni binafasi kutoka nchini humo kuja kuwekeza katika
viwanda na miundombinu ya vuvuvi ili kuongeza uzalishaji
kupunguza upotevu wa rasilimali za uvuvi na kuongeza ubora na
usalama wa mazao ya uvuvi hapa nchini.


“Zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanajishughulisha na shughuli
mbalimbali katika mialo, na sekta ya uvuvi inawapatia kipato na
lishe wananchi na kuchangia pato la taifa.”alisema Waziri Ndaki
Asilimia 85 ya mazao ya uvuvi yakiwamo yale yanayosafirishwa nje ya nchi yanatokana na wavuvi wadogo wadogo ambao hutumia vyombo vidogo vya kuanzia mita tatu hadi mita 10.


Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wavuvi katika mwalo wa
Chato Beach, Kamese Kalima alisema mwalo huo umeanzishwa mwaka 1999 ukiwa na wavuvi 500 na mitumbwi 125, na kati ya hiyo mitumbwi 110 ni ya makasia na mitumbwi 15 ni ya injini.


Bw. Kalima aliiomba Serikali ya China kuwasaidia kutatua
changamoto za miundombinu zinazowakabili ambazo ni
vyombo vya uvuvi, jengo ambalo litajumuisha soko la uvuvi,
mitambo ya kuzalisha tani 5 za barafu, chumba cha ubaridi
chenye uwezo wa kuhifadhi tani 10 za samaki, na mashine ya
umeme yenye uwezo wa kukaushia tani 5 za dagaa kwa siku.


“Tunatambua China ni vinara wa viwanda vya samaki duniani,
hivyo tunaomba miundombinu ya uchakataji samaki na China
kuja kuwekeza viwanda vya kuchakata samaki angalau tani 35
kwa siku.” Alisema Bw. Kalima.

Mwalo wa Chato na Mkoa wa Geita kwa ujumla unazalisha
zaidi ya tani 23,844 za samaki kwa mwaka ambao husafirishwa
umbali mrefu kwenda viwanda vilivyopo Kagera na Mwanza
kwa ajili ya kuchakata samaki.

No comments:

Post a Comment

Pages