HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2021

Zimamoto wakusanya Bilioni 81


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (watatu kushoto) akimsikiliza Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Gilbert Mvungi (wanne kushoto)  akimpa maelezo ya chanzo cha maji kinachoonekana pichani kinachotumika  wakati wa tukio la kuzima moto  na uokozi wakati wa ziara ya kikazi ya naibu waziri huyo kutembelea Makao Makuu ya jeshi hilo leo jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 

Na Mwandishi Wetu

 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 81,336,956,451 katika kipindi cha miaka mitano ikiwa ni gharama za ukusanyaji wa tozo za ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto katika majengo 356,845 nchi nzima ikijumuisha viwanda, mahoteli, mashule, masoko, migodi, maduka, hospitali, maofisi, matenki ya mafuta, nyumba za kuishi na vyombo vya usafiri.

 

Hayo yamesemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati wa ziara ya kikazi Makao Makuu ya jeshi hilo,leo jijini Dodoma.

 

“Kwa kuwa ukaguzi huo wa king ana tahadhari ya moto huenda sambamba na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali,Jeshi limefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 81,336,956,451,aidha,Jeshi la Zimamoto linaendelea na jitihada za kuboresha maduhuli ikiwa ni Pamoja na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa makusanyo ambao utasaidia kupunguza upotevu wa maduhuli ya serikali” alisema Kamishna Masunga.

 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo alilipongeza jeshi hilo huku akitaka waongeze ufanisi ikiwepo kufika kwa haraka katika matukio ya moto ili kuweza kunusuru Maisha na mali za wananchi.

 

“Kumekuwepo na malalamiko juu ya askari wetu kuchelewa kufika katika maeneo ya moto au ajali yoyote ili kufanya maokozi,nawasihi kufika haraka katika matukio mbalimbali kwani wananchi wanawategemea na uwepo wenu unasaidia mambo mengi kwa kuwa nyie ndio mna utaalamu na udhibiti wa majanga ya moto na uokozi” alisema Naibu Waziri Khamis Hamza Chilo.

 

Sambamba na mafaniko hayo jeshi hilo pia limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Jengo la Makao Makuu jijini Dodoma,Kituo cha Zimamoto na Uokoaji katika Wilaya ya Chato mkoani Geita,linaendelea na ujenzi wa kituo cha zimamoto wilayani Chamwino na ujenzi wa nyumba za askari wake katika eneo la Kikombo jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Pages