HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2021

Bilioni tisa zilivyotekeleza sera ya utoaji elimu bila malipo mkoani Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.

 

Mkoa wa Ruvuma umepokea shilingi 9,205,781,600.28 ili kutekeleza sera ya utoaji elimu bila malipo katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba 2019 hadi Novemba 2020.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema fedha hizo zimesaidia kuongeza kiwango cha uandikishaji na mahudhurio ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na kuongezeka upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada.

“Utekelezaji wa sera hii umeweza kuleta unafuu kwa wazazi na walezi katika kugharamia gharama za elimu kwa watoto wao’’,alisisitiza Mndeme.

Mndeme amesema Mkoa umeendelea kuimarisha utoaji wa elimu katika ngazi zote na kwamba Mkoa wa Ruvuma umepata mafanikio makubwa baada ya serikali kujenga vyuo viwili  vipya vya ufundi stadi VETA na kuufanya Mkoa kuwa na vyuo vitatu vya VETA.

Hata hivyo amesema Mkoa hivi sasa unaweka msukumo mkubwa katika utoaji wa taaluma bora kwa kuwashirikisha wadau wote wa elimu ili kuhakikisha kila mdau anashiriki kufanikisha tendo la ufundishaji,ujifunzaji na mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

 “Kwa niaba ya wananchi,naishukuru serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu Mhe.Dkt.John Magufuli kwa kuendelea kufanya elimu kuwa kipaumbele ambapo serikali imeamua kila Mkoa,ukiwemo Mkoa wetu kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana ya kitaifa’’,alisema Mndeme.

 Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 808 kati ya hizo,shule za serikali ni 778 na zisizo za serikali 30,pia Mkoa una shule za sekondari 206 kati ya hizo za serikali ni 150 na sekondari binafsi 56.

No comments:

Post a Comment

Pages