Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku akitoa wasilisho la Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kwa wadau kutoka katika jamii za pembezoni katika kikao cha majadiliano baina ya Wizara hiyo na wadau hao kilichofanyika, jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi kutoka Baraza la wanawake wafugaji wa jamii ya kimasai Sarah Alakara akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali baina ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na jamii za pembezoni kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Na Faraja Mpina- WMTH
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya majadiliano na wawakilishi wa makundi mbalimbali kutoka katika jamii za pembezoni ambao ni wawindaji, wafugaji, wakusanya matunda na warina asali wa asili ili kujadili namna bora ya kutekeleza Mradi wa Tanzania ya kidijitali kwa kuepuka athari za kimazingira katika jamii hizo zinazotegemea mazingira katika kuendesha maisha yao ya kila siku.
Majadiliano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam, kwenye kikao baina ya Wizara hiyo, wawakilishi wa makundi hayo na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa Wizara ipo katika maandalizi ya kutekeleza Mradi wa Tanzania ya Kidijitali utakaoanza rasmi mwezi Julai mwaka huu na moja ya vitu muhimu inavyoangalia ni kuhakikisha mradi huo unakuwa jumuishi ili usilete athari kwenye mazingira na jamii kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo ni mpango wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano ya simu popote nchini na kuongeza idadi ya matumizi ya intaneti kutoka asilimia 46 ya sasa hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2025 ili wananchi waweze kushiriki katika uchumi wa kidijitali kwa kutumia fursa nyingi zinazopatikana kupitia matumizi ya intaneti.
“Kuna maeneo wananchi wanaweza kupiga simu tu bila kupata huduma nyingine zinazotumia intaneti kutokana uwepo wa minara yenye teknolojia ya 2G isiyoakisi mahitaji yaliyopo katika maeneo hayo. Mradi huu unaenda kuboresha matumizi ya teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili wananchi waweze kupata huduma nyingine za ziada”, Munaku
Naye Rogasian Lukoa kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali utazingatia haki na utu wa jamii za pembezoni na zinazotegemea mazingira katika kuishi kwa kubainisha mila na desturi zao na kuboresha jamii hizo ili ziweze kuendelea.
“Kuna miongozo mbalimbali katika utekelezaji wa Mradi huu ambayo inaonesha namna bora za kuepuka kwa kadri inavyowezekana athari za kimazingira ili kulinda maslahi ya jamii hizo”, Lukoa
Kwa upande wa mwakilishi kutoka Baraza la wanawake wa kifugaji kutoka Mkoa wa Arusha Sarah Alakara amesema kuwa mradi huu utakuwa na matokeo makubwa kwa jamii iwapo maeneo yenye uhitaji zaidi yakipewa kipaumbele ili kwenda nao pamoja katika kuhakikisha wananufaika na shughuli mbalimbali wanazozifanya kupitia njia rahisi ya teknolojia ya dijitali.
Alisisitiza kuwa kuna baadhi ya maeneo ya jamii za pembezoni ambayo hayana mawasiliano ya simu za mkononi mpaka waende vijiji vya jirani ndio waweze kupata mawasiliano hayo.
Naye Honest Njau Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema kuwa pamoja na mambo mengine mradi huo una lengo la kupeleka mawasiliano kwa jamii ya kitanzania pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali ili Serikali iweze kufanya maunganisho na taasisi zake lakini pia kupeleka na kuboresha mawasiliano katika maeneo ya mijini,vijijini na pembezoni.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment