HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2021

SERIKALI ZA VIJIJI ZATAKIWA KUWATAMBUA VIJANA WENYE UJUZI MBALIMBALI

Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani, akiangalia kazi za wahitimu wa mafunzo ya ufundi  katika Kata  ya Kinyangege na Ulemo wilayani  Iramba mkoani Singida.

Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani ( kushoto) akizungumza na  vijana waliohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi.  

 Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu na viongozi mbalimbali.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akikabidhi vyeti.


Na Dotto Mwaibale, Singida


KAIMU Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amezitaka Serikali za Vijiji, Mitaa na Kata kuwatambua vijana wote wenye ujuzi wa ufundi mbalimbali.

Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa kauli hiyo kwenye mahafali ya wahitimu elimu ya ufundi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kata ya Kinyangege wilayani Iramba mkoani humo.

Alisema Serikali imekuwa ikituma fedha za ujenzi na shughuli mbalimbali katika maeneo yenye kazi mfano ujenzi wa miundombinu ya shule kama mabweni, madarasa, hospitali na vituo vya afya lakini viongozi badala ya kuwapatia kazi vijana walio katika maeneo yao wao wanachukua mafundi kutoka maeneo mengine.

Ndahani aliongeza kuwa pia  wakati mwingine fundi mmoja anaweza kuwa na kazi zaidi ya mbili katika vijiji tofauti kuwa utaratibu huo haukubaliki kwani  lengo la Serikali la kutumia Force Account katika kazi hizo ni kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.

"Ukisha watambua vijana wenye ujuzi ni rahisi kuwapatia kazi  katika maeneo walipo." alisema Ndahani.

Aidha  Ndahani aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa na kujali masilahi ya Taifa kwani  mengi yamepata ufadhili kutoka nje ya nchi hivyo wahakikishe kuwa ufadhili huo  usije kuathiri Taifa kwa namna yoyote kupitia masharti yao.

Alisema kuna taarifa katika nchi za jirani  kuwa mashirika yalitumika kuvuruga amani, mshikamano na usalama wa  nchi ambapo aliliomba  Shirika la SEMA ambalo limetoa ufadhili wa mafunzo hayo kwa vijana kuwa makini ili  heshima walioijenga katika mkoa huo na Taifa isije kutoweka.

Ndahani aliwataka vijana waliopata ujuzi mbalimbali katika Kata hiyo ya Kinyangege na Ulemo wilayani humo kuonesha kwa vitendo ujuzi wao badala ya kujifungia ndani huku wakilalamika kuwa hawana ajira.

 Katika mahafali hayo jumla ya vijana 157  ikiwa wavulana 98  na wasichana 58 walihitimu mafunzo ya ufundi stadi katika fani ya ushonaji, upishi, uhunzi , kilimo, urembo na ususi , useremala na ujenzi kwa ufadhili wa Shirika la SEMA na SROMME kupitia miradi ya BONGA NA TUNAWEZA.

Kwa upande wao Vijana wamelishukuru Shirika la SEMA kwa kuwapatia ujuzi na kuahidi kutumia majukwaa ya vijana ili kujikwamwua na umasikini.

No comments:

Post a Comment

Pages