HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2021

UTT AMIS YASHIRIKI MAONYESHO YA MIFUKO YA UWEZESHAJI, KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOZUIA WANANCHI KUWEKA AKIBA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati akifungua Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji  Wananchi  kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abei jijini Arusha, leo Februari 9, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Ofisa Masoko na Uhusiano wa Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Martha Mashiku, wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho   ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi  kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mmoja wa wananchi akipata huduma katika banda la Kampuni ya UTT AMIS.
Wawakilishi wa madiwani kutoka kata za Arusha Mjini wakiwa katika banda la UTT AMIS.
 
 
Arusha, Tanzania 
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Jumanne, Februari 9, 2021  amefungua Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi yanayoendelea katika Viwanja vya Shiekh Amri Abied jijini Arusha.

Katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza mifuko na programu zote za uwezeshaji zifanye tathmini ya shughuli na huduma zake ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji uboreshaji hususan eneo la masharti ya utoaji mikopo kwa wajasiriamali.

Pia, Waziri Mkuu ameitaka mifuko inayotoa dhamana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali nchini, iimarishe usimamizi, uratibu na utendaji wake kwa kutengeneza mipango maalum ya kila mwaka inayoonesha malengo ya dhamana zitakazotolewa katika mwaka husika.
 
Amesema mipango maalumu itakayoandaliwa na mifuko inayotoa dhamana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali inatakiwa iwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na baadaye taarifa za utekelezaji zitolewe katika kipindi cha kila robo mwaka.
 
“Wasimamizi na Watendaji wa mifuko na programu pamoja na walengwa jiepusheni na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. Pia, watendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji pamoja na taasisi za fedha hakikisheni mnatoa huduma bila urasimu wala ubaguzi wa aina yoyote. Nasisitiza wananchi wanapofika kwenye ofisi zenu wapokelewe kwa staha, wasikilizwe na kupatiwa huduma stahiki kwa wepesi.”
 
Aidha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  amezitaka Halmashauri nchini zihakikishe zinatenga asilimia 10 ya mapato yake ya fedha za ndani ili zitumike kutoa mikopo kwa vijana (asilimia 4), wanawake (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2). Pia, ametoa wito kwa Mabaraza ya Madiwani katika kila Halmashauri kufuatilia utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ambayo yameridhiwa na Bunge na kutungiwa sheria mahsusi.”


Aidha Waziri Mkuu ameagiza mifuko na programu zinazowawezesha wananchi kiuchumi zifanye tathimini ya kubaini changamoto  na maeneo yanayohitaji maboresho hasa katika utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa vyombo mbalimbali vya habari kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo ili viweze kufikisha ujumbe sahihi kuhusu fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mifuko na programu za uwezeshaji kwa wananchi wote nchini.

Amesema tathmini za mara kwa mara zinazofanywa na Serikali kuhusu utendaji wa Mifuko na Program za Serikali za uwezeshaji zinaonesha kwamba mifuko hiyo na programu hizo zimechangia kwa kiwango kikubwa jitihada zake za kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

“Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 mifuko na programu za uwezeshaji za Serikali zimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.22 na hivyo, kunufaisha zaidi ya watu milioni 4.9 na taasisi 5,499.”

Waziri Mkuu amesema sambamba na programu na mifuko hiyo, Halmashauri 185 Tanzania Bara zimefanikiwa kutoa shillingi bilioni 93.3 kupitia mifuko ya uwezeshaji wa makundi maalum ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Fedha hizo, zimewezesha upatikanji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 32,553.

“Nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba kila halmashauri ihakikishe inatenga asilimia 10 ya mapato yake ya fedha za ndani ili zitumike kutoa mikopo kwa vijana (asilimia 4), wanawake (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2)”

Katika hatua nyingine Waziri mkuu ametoa wito kwa Mabaraza ya Madiwani katika kila Halmashauri kufuatilia utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ambayo yameridhiwa na Bunge na kutungiwa sheria mahsusi.”

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amesema baraza hilo linajukumu la kusimamia, kufuatilia na kuratibu shughuli mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo mifuko na programu za uwezeshaji.

“Mifuko hii imeanzishwa kwa ajili ya kutatua changamoto zinazozuia wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, ambazo ni pamoja na ufinyu wa vyanzo vya akiba na mapato, kutokuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba, kuwepo kwa masharti magumu ya mikopo, ukosefu wa mitaji, ukosefu wa dhamana na riba kubwa zinazotozwa na mabenki kwenye mikopo,” amesema.

Amesema, baraza linaratibu mifuko na programu za uwezeshaji zipatazo 55, ambapo kati yake mifuko ni 48 na programu saba. Uratibu unaofanywa ni pamoja na kutunza daftari la orodha ya mifuko, kufanya mikutano na taasisi zenye mifuko na programu za uwezeshaji, kupokea taarifa za mifuko na kujenga uelewa kwa umma juu ya uwepo wa mifuko na programu hizo. 

No comments:

Post a Comment

Pages