Mwakilishi wa Jimbo la Wingwi Kombo Mwinyi Shehe akimkabidhi Unifomu za wanafuni 60 wa Jimbo hilo ambao wamefaulu michepuo wakiwemo saba wa kupawa maalum Afisa mdhamini elimu Pemba Mohamed Nassor salim na kisha mdhamini kukabidhi mmoja kati ya wanafunzi hao katika Shuhuli iliyofanyika Skuli ya wingwi Wilaya ya Micheweni kaskazini Pemba.
MWAKILISHI wa Jimbo la Wingwi Kombo Mwinyi Shehe, ameanza kutekeleza ahadi yake, kwa upande wa sekta ya elimu, baada ya kuwazawadia wanafunzi 60 waliofaulu kwa madarasa ya nne na sita wa jimbo hilo.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi hizo, kwenye sherehe zilizofanyika skuli ya Wingwi, alisema wakati alipokuwa akiomba ridhaa, aliahidi kufanya hivyo kama akipata ridhaa.
Alisema, sasa ni wakati wa kutekeleza ahadi zake mbali mbali alizoziweka, na kusema anachohitaji ni ushirikiano kutoka kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Alieleza kuwa, kuwazawadia wanafunzi hao ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake, ambazo alisema hilo litakuwa ni jambo endelevu kwa kipindi chote cha uongozi wake.
“Leo natimiza ahadi yangu ya kuwazawadia wanafunzi hawa waliofaulu, maana wakati naomba ridhaa, niliahidi kuwapa zawadi watakaofaulu ngazi ya michepuo na vipawa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mwakilishi huyo wa Jimbo la Wingwi Kombo Mwinyi Shehe, alisema anatarajia kukaa na waalimu wote wa skuli za Jimbo hilo, ili kuona anandaa mitihani maalum.
Alisema mitihani hiyo, inalengo la kuwapima wanafunzi ambayo itakuwa kwa madarasa yote yanayojiandaa kwa mitihani ya taifa na gharama zote atazibeba.
“Katika kuhakikisha Jimbo la Wingwi linapiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwenye sekta ya elimu, nitandaa mitihani kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya taifa,’’alieleza.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi hao wanaokwenda skuli za nje ya jimbo hilo, kuendelea na masomo yao, kuzingatia zamira zao na sio kushughulikia anasa.
Mapema Afisa Mdhamini wizara ya Elimu Pemba, Mohamed Nassor Salim, amemtaka Mwakilishi huyo kufanya kila mbinu, kuhakikisha anakuza sekta ya elimu Jimboni mwake.
Aidha amewataka wazazi na walezi, kupunguza matumizi yasiokuwa ya lazima, na kutenga fedha kwa ajili huduma ndogo ndogo kwa vijana wao.
“Na nyinyi wanafunzi muelewe kuwa, wazazi wenu wamekuwa wakipoteza nguvu kubwa kuhakikisha nyinyi mnaishi kwenye mazingira rafiki ya kupata elimu, hivyo jitahidini,’’alisema.
Kwa upande wake Msaidizi Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Maandalizi na msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni Tarehe Khamis Hamad, alisema ushirikiano baina ya wazazi na waalimu, ndio mwarubaini wa kukuza elimu.
Aidha alimpongeza Mwakilishi huyo wa Jimbo la Wingwi, kwa uungwana wake, wa kutekeleza ahadi yake ya kuwazawadia wanafunzi wote waliofaulu.
Mmoja kati ya wanafunzi aliyefaulu kipawa maalum, Fatma Amour wa skuli ya Sizini alisema utekelezaji wa ahadi kwa Mwakilishi huyo, kumewapa moyo wa kusoma zaidi.
Katika hafla hiyo, jumla ya wanafunzi 60 wa madarasa ya nne na sita kutoka skuli za Sizini, Wingwi, Simai na Mtemani walikabidhi sare za skuli kutoka kwa Mwakilishi huyo, zenye thamani ya shilingi milioni 1.8.
No comments:
Post a Comment