HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 13, 2021

NAIBU WAZIRI KATAMBI ATAKA MIKOPO YA NYUMBA ILENGE WANANCHI WA KIPATO CHA CHINI

Na Zubedah Mtemi Ramadhani, ARUSHA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi ametoa wito kwa mifuko ya uwezeshaji ujenzi wa  nyumba kuhakikisha inatoa mikopo  kwa wananchi wa kipato cha chini ili kuwawezesha kujenga nyumba bora katika maeneo yaliyopangwa na hivyo  kupunguza ujenzi holela.

Katambi alitoa wito huo leo tarehe 13 Februari 2021 wakati akifunga maonesho ya nne ya mfuko wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Alisema, Wizara ya Ardhi kupitia Mfuko wa Nyumba ikijenga  nyumba katika mpangilio na kuwakopesha wananchi itawasaidia wananchi wenyewe kupata makazi bora na wakati huo kuepusha ujenzi holela katika maeneo mabalimbali.

"Mufuko hii itasaidia sana wananchi kupata nyumba katika maeneo yaliyopangwa na kupimwa na hivyo kuepusha ujenzi holela" alisema Katambi.

Aidha, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira aliipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa na kuuelezea uamuzi huo kwamba umesaidia kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi na kutolea mfano wa utoaji wa hati za ardhi unafanyika kwa haraka na kwa wakati.

Akigeukia suala la viwanja visivyoendelezwa katika maeneo mbalimbali ambavyo baadhi yake vimegeuka kuwa pori, Katambi ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha inafuatilia ili kupunguza maeneo mengi yasiyoendelezwa. 

Maonesho ya nne ya mfuko wa Programu za Uwezeshaji Wananchi  Kiuchumi yalianza tarehe 7 Februari 2021 na kufunguliwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ambapo yalihusisha  mifuko na programu za uwezeshaji 25 , taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi zinazofanya shughuli za kuwezesha wananchi kiuchumi 77 pamoja na wajasiriamali 200 kutoka katika halmashauri mbalimbali  na kutoka katika mikoa ya kanda ya kaskazini.

No comments:

Post a Comment

Pages