Baadhi ya wadau wakiwa katika Kikao Kazi.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Abubakar Kunenge aipongeza Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa mikakati ya kusaidia jitihada za Serikali katika kutunza na kuboresha mazingira. Mhe. Kunenge aliyasema hayo katika mkutano wake na watendaji wa serikali ngazi ya kata na mitaa uliofadhiliwa na Benki ya CRDB.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na watendaji kutoka Wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine mkutano huo ulilenga zaidi katika kuhimiza uwajibikaji na utekelezaji wa maagizo ya serikali katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, usafi wa mazingira, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, umeme, maji safi na maji taka ili kutatua kero mbalimbali za wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.
Mh. Kunege aliishukuru Benki ya CRDB kwa kudhamini mkutano huo huku akipongeza benki hiyo kwa kampeni ya Pendezesha Tanzania iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka 2020 ambayo imelenga kuboresha muonekano wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na upandaji wa miti.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana Benki ya CRDB kwa kushirikiana kwa karibu na serikali ya mkoa wa Dar es Salaam katika kufanikisha mkutano huu ambao moja ya agenda zake ni kujadili namna bora ya kuboresha usafi wa mazingira ya jiji letu la Dar es Salaam” alisema Mh. Kunenge.
Pamoja na kugusia suala la usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa aliweka mkazo zaidi katika suala la ufanisi waukusanyaji mapato huku akiwasisitiza watendaji kusimamia nidhamu ya matumizi ili mapato hayo yakaweze kuonekana na kuleta tija kwa wananchi. Vile vile Mkuu wa Mkoa alisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato unapaswa kwenda sambamba na kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia wafanyabiashara.
Sambamba na agenda za kuhusu kuboresha utendaji, vile vile watendaji wa serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam pia walipata fursa ya kupata elimu ya masuala ya fedha kutoka Benki ya CRDB.
No comments:
Post a Comment