HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 13, 2021

VIKUNDI VITAKAVYOSHINDWA KUFANYA MAREJESHO YA FEDHA ZA MIKOPO KUFIKISHWA MAHAKAMANI


 Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Murshid Issa, akizungumza na wajasiriamali.

 

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Jumla ya Vikundi 30  vya waliotoa mikopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kushindwa kufanya marejesho ya fedha za mikopo hiyo, shauri la madai linakusudiwa kupelekwa mahakamani endapo muafaka hautapatikana.

Kauli hiyo imetolewa na  Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Murshid Issa, wakati akizungumza na wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wauzaji wa senene, wauzaji wa mboga mboga na wakulima katika ukumbi wa ELCT Manispaa ya Bukoba katika semina iliyoambatana na tamasha la SENENE FESTIVAL  lililolenga maonyesho ya biashara na huduma ili kuongeza thamani ya kupanua masoko lililoandaliwa na COSTOMER SATISFACTION DEVELOPMENT LIMITED chini ya Mkurugenzi na mwanzilishi  Emmanuel Cypriani Mwombeki.

Hatua hiyo imekuja kufuatia wajasiriamali hao akiwemo Josephina Ansibert  mfanyabiashara wa senene kuhoji afisa maendeleo ya jamii juu ya kikundi kilichoundwa cha wajasiriamali wa senene na kisha kuishia kusikojulikana.

Akijibu swali hilo Murshid  amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali walio wengi wanashindwa kutafuta taarifa ili kujua mikopo inavyokwenda ili kubaini faida na hasara ikiwemo kukwepa semina mbalimbali zinazotolewa wengi wao wakitanguliza maslahi kuliko kujifuza.

Amesema kuwa  mwaka 2019 hadi 2020 halmashauri hiyo imetoa takribani mikopo ya  milioni 330 kwa vikundi 46 ambapo Kati ya fedha hizo asilimia 10 ilikuwa milioni 182 na iliyobaki ilikuwa marejesho kutoka kwenye vikundi vyenye mikopo na mwaka huu wametoa kwa asilimia 100.

Amesema kuwa kwa mwaka 2021 halmashauri hiyo imelenga kufikia vikundi 46 ambapo Hadi sasa wako na vikundi 23.

"Changamoto upande wa marejesho vikundi vingi ushindwa kurejesha kwa wakati walio wengi wakidai shughuli zao zilikumbwa na janga la Corona kundi la  walemavu nalo halifanyi marejesho Kama inavyotakiwa jambo ambalo hukwamisha fursa kwa makundi mengine kupata mikopo hivyo nasema dawa ya Deni ni kulipa hivyo kwa mujibu wa kanuni yetu ya mikopo inaturuhusu kwamba mtu asipofanya marejesho na tukishindwa kuhafikiana basi shauri la madai linapelekwa mahakamani "alisema Murshid.

Ameongeza kuwa tayari siku 14 zimeishatolewa kwa vikundi ambavyo havijafanya marejesho kufaya hivyo haraka ili wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Aidha afisa maendeleo ya jamii amewataka akina mama na vijana kuendelea kutumia fursa ya kujipatia mikopo na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwani serikali ya awamu ya tano imelenga kuwakwamua  kiuchumi.

 Kwa upande wake Emmanuel Cypriani Mwombeki ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Costomer Satisfaction  Development Limited amesema kampuni hiyo imejikita katika kushughulika na ujasiliamali, kuboresha huduma kwa wateja  kuangalia fursa za uwekezaji ikiwemo vivutio vya utalii, tamaduni za Mkoa wa Kagera na kueleza kuwa wameamua kuandaa tamasha hilo ambalo limewakutanisha wadau wote wakiwemo TRA, Brela, TBS, SIDO taasisi za kifedha pamoja na taasisi za kiserikali huku akiiomba serikali na wadau mbalimbali kuunga mkono pale yanapoletwa matamasha kama hayo.

Hata hivyo wajasiriamali hao wakiwemo wauzaji wa senene wameiomba serikali kuwaboreshea eneo la kuuzia biashara yao ya senene kwani wamekuwa wakikumbana na changamoto ikiwemo kunyeshewa mvua huku wakitaja kuchukua bidhaa hiyo kwa bei ya juu na kulalamikiwa na wateja kutokana na msimu huu kukosa senene.

No comments:

Post a Comment

Pages