HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 30, 2021

MKAZI WA BUKOBA AUA MKE NA MTOTO KISHA AJINYONGAA

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vifo vya watu watatu.

 

 Alodia Dominick, Bukoba

BABA wa familia Sudi Mwamandi (49) mkazi wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera amejinyonga hadi kufa baada ya kutekeleza mauaji ya mke wake na mwanaye kikatili kwa kuwakata  mapanga kwa sababu ya kubadili dini.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi akiongea na waandishi wa habari Machi 30, 2021  amewataja marehemu hao kuwa ni Editha Martin (48) mkulima na binti yake Pili Sawia (25) na baba wa familia hiyo Sudi Mwamandi (49) ambaye anadaiwa kujinyonga baada ya kutekeleza mauaji ya mkewe na binti yake.

Kamanda Malimi amesema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mayondwe Wilaya ya Muleba machi 26, 2021 ambapo Editha na Sawia walibarilisha dini yao ya mwanzo kutoka uislam na kuwa wakristo jambo ambalo lilipingwa na mtuhumiwa na kusababisha kutokea ugomvi mara kwa mara hali iliyopelekea Editha na Sawia wahame nyumba na kwenda kuishi sehemu nyingine.

Amesema siku ya Machi 26 mwaka huu usiku saa tisa ndipo mtuhumiwa alikwenda kwenye nyumba alipohamia mkewe na binti yake na kuvamia akamkuta marehemu mkewe peke yake na kuanza kumshambulia kwa  kitu chenye ncha kali sehemu za mwili wake na kumkata kwa panga na kusababisha kufariki dunia na baada ya kutekeleza tukio hilo alianza kukimbia kutoka eneo hili ndipo alikutana na binti yake njiani naye alimkata sehemu mbalimba za miwili kwa panga na kupoteza maisha papo hapo.

"Kutokana na uchunguzi wa awali inaonekana baada ya kusababisha matukio hayo  mtuhumiwa alijitundika juu ya mti ulioko katika eneo hilo na kujinyonga kwa kutumia shuka, nawataadhalisha wananchi na kuwataka waache kabisa tabia ya kujichukulia sheria mikononi pia kutowanyanyasa wanawake kijinsia maana katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu kila mtu kuabudu kwa imani anayoipenda hivyo, kumzuia mtu ni kosa kikatiba"amesema Malimi.

Wakati huo huko kamanda Malimi alisema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja anayeitwa Kusekwa Madaha (27) mkulima wa kijiji cha Mulongo Wilayani Kyerwa kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la nne (15) hivyo, kutokana hari hiyo kamanda alieleza kuwa jeshi hilo litawasaka kwa nguvu zote wale wanaowabaka wanafunzi nakuwapa mimba kwani mtu anayefanya hivyo ni sawa na anayejihusisha na madawa ya kulevya.

No comments:

Post a Comment

Pages