Na Dotto Mwaibale, Singida
KATA ya Dung'unyi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imetekeleza agizo la Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza madawati na kuhakikisha wanafunzi wote walioanza kidato cha kwanza mwaka huu wanakwenda shuleni na wanakaa kwenye viti.
Madawati hayo yamepatikana kutokana na nguvu za wananchi.
Akizungumza jana wakati akikabidhi madawati hayo Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Yahaya Njiku aliwapongeza wananchi kwa kutengeneza madawati hayo kwa nguvu zao.
Alisema hatua hiyo waliifikia kufuatia ongezeko kubwa la ufaulu wa watoto na kuhakikisha wote wanakwenda shuleni na kuwa na viti vya kukalia.
" Leo nakabidhi madawati mapya 18 hapa Shule ya Sekondari Munkinya katika kata hii ya Dung'unyi ikiwa ni awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukabidhi madawati 20 na idadi ya madawati yote kufikia 38 huku madawati zaidi ya 70 yakikarabatiwa." alisema Njiku.
“Kwa nchi nzima halmashauri yetu imekuwa ya 78 kati halmashauri 195 zilizopo kwa kutengeneza madawati tunakila sababu ya kujivunia na naamini kabisa ipo siku na sisi tutashika nafasi ya kwanza” alisema.
Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari ya Munkinya, Faraja Mlelwa aliwashukuru wadau wa maendeleo waliochangia upatikanaji wa madawati hayo na kuwa watayatunza.
Lengo la halmashauri hiyo ni kuhakikisha madawati yote 3900 yanayohitajika yanapatikana na kuwa watoto wote wanafika chuo kikuu.
No comments:
Post a Comment