Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na baadhi ya wanahabari mara baada ya hafla hiyo. |
KAMANDA wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amewataka wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika familia zao wajitokeze na kudai haki zao mbele ya sheria, badala ya kuendelea kukaa kimya kwa kilea kinachodaiwa wanaona aibu huku wakizidi kuteseka.
Kamanda Mambosasa ametoa wito huo juzi katika Kata ya Pangani Ilala jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga awamu ya pili ya huduma za mkono kwa mkono maarufu 'Ones Stop Center' zinazotembea kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika kata tisa za Mkoa wa Kipolisi wa Ilala takribani kwa siku 18.
Pamoja na hayo aliongeza kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na unyanyasaji watoto vikiwemo vya ubakaji, ukeketaji, utumikishaji watoto na ndoa za utoto vinavyowanyima watoto haki zao haviwezi kukubalika, kwani watoto hao ndio viongozi na wajenzi wa taifa la kesho.
“Watoto wa sasa ndio akina Rais Samia Suluhu wa kesho; ndio akina Lazaro Mambosasa wa kesho; ndio madkatari na viongozi wa kesho hivyo, lazima haki zao zilindwe na waendelezwe.” Hivyo, lazima Watanzania tuungane na kusimama pamoja kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa ili kesho na kesho kutwa, washike nafasi mbaimbali kutumikia taifa,” alifafanua Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa aliipongeza taasisi ya Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha huduma za mkono kwa mkono zinazotembea na kuahidi kuendelea kuunga mkono na kusaidia kufanikiwa zaidi kwa huduma hizo ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia eneo lake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Program wa Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai akizungumza katika hafla hiyo, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada za kupambana na uhaifu ukiwemo ukatili wa kijinsia, na hasa utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo pamoja na kutoa elimu na huduma dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Alisema hatua hiyo inaifanya jamii kuongeza imani yake kwa polisi hivyo, kujitokeza kueleza kero zao zikiwamo za kifamilia.
“Kitendo cha polisi kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kusikiliza kero zao sambamba na kuwapa msaada ukiwamo wa kisheria, msaada wa kipolisi, unasihi na huduma za afya na elimu dhidi ya ukatili wakijinsia, kinaonesha uhusiano mwema baina ya polisi na raia unazidi kuimarika. Bado wadau wote kwa pamoja tuna kazi kubwa mbele yetu na sisi tunaahidi kuendelea kushirikiana na polisi kadiri inavyowezekana.” Alisema Bi. Swai.
Naye Mratibu wa One Stop Center katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk Christina Onyango, alisema mbali na vituo hivyo kutoa huduma za upimaji afya kama macho, sukari na shinikiza la damu, unasihi, huduma za kisheria, pia wananchi wamekuwa wakifundishwa namna ya kubaini, wahusika, dalili, aina na namna ya kuripoti na kutunza ushadidi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Dk. Onyango alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya huduma kama hizo ilifanyika Desemba mwaka jana katika kata saba zilizo katika mkoa huo wa kipolisi ikiwa ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Baadhi ya wananchi wakihudumiwa kwenye huduma za mkono kwa mkono maarufu 'Ones Stop Center' zilifofanyika eneo hilo. |
No comments:
Post a Comment